Mwanza. Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakati wa alfajiri unapokaribia, mamilioni ya Waislamu huamka usingizini kushiriki ibada ya kipekee inayojulikana kama daku. Ni tukio linalojirudia kila siku kwa mwezi mzima, likiwaunganisha waumini katika ibada, nidhamu na maandalizi ya swaumu ya siku inayofuata.

Kwa wengi, daku huchukuliwa kama mlo wa kuzuia njaa ya mchana. Hata hivyo, katika mafundisho ya Uislamu, daku si chakula tu bali ni Sunna iliyojaa baraka, yenye kuunganisha mahitaji ya mwili na ya roho. Ni alama ya utambulisho wa swaumu ya Muislamu na ni muda wa kipekee wa ibada, dua na utulivu wa nafsi.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake), daku imehimizwa wazi. Katika hadithi iliyopokelewa na Anas bin Malik (R.A), Mtume amesema: “Kuleni daku, kwani hakika katika daku kuna baraka.” (Imepokewa na Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim).

Kauli hii inaweka bayana kuwa daku ni zaidi ya mlo; ni kitendo cha utiifu chenye kumletea mfungaji nguvu za kimwili na kiroho katika kutekeleza ibada ya swaumu.

Katika mihadhara na darsa mbalimbali, wanazuoni wamekuwa wakikumbusha kuwa baraka za daku hujidhihirisha kwa namna nyingi. Mfungaji anayekula daku hupata wepesi wa kutekeleza ibada nyingine mchana, ikiwamo kusoma Qur’an, kuswali na kujizuia na hasira licha ya njaa.

Mwalimu wa dini, Issa Pangara, anasema kula daku ni kufuata Sunna na ni alama inayotofautisha swaumu ya Muislamu na asiye Muislamu, kama ilivyopokelewa katika hadithi ya Imam Muslim.

Anabainisha kuwa hata kama mtu hana hamu ya kula, kunywa maji au kula tende chache kunatosha kupata fadhila za daku. Aidha, anataja kuwa muda wa daku ni miongoni mwa nyakati zinazokubaliwa dua, hivyo kumpa muumini fursa ya kuunganisha lishe ya mwili na lishe ya roho.

Imamu wa Msikiti wa Al-Aqaba, Isamilo jijini Mwanza, Muhammad Omar, anaeleza kuwa muda wa daku huanzia nusu ya usiku hadi kabla ya alfajiri ya kweli. Anasema huo ni wakati wa baraka unaompa mfungaji nguvu na subira ya kuhimili siku.

“Wanachuoni wameeleza kuwa wakati wa kula daku ni kuanzia nusu ya usiku mpaka kabla ya alfajiri ya kweli. Ni muda wa baraka… kama Allah alivyosema, ‘Kuleni na kunyweni mpaka itakapochomoza alfajiri ya kweli.’ Hili humletea mfungaji nguvu tofauti na yule ambaye hakula daku,” anasema.

Naye Sheikh Hudhayfa Ayman wa Masjid Sunnah Tanga anaeleza kuwa daku husaidia kudhibiti hulka zinazoweza kuchochewa na njaa kama ukali na hasira.

“Mtu anapokuwa na njaa anaweza kuwa na hulka ya ukali. Daku hupunguza hali hiyo na kumsaidia mfungaji kuwa mtulivu. Pia ni fursa ya kumtaja Allah kwani  unaanza kwa ‘Bismillah’ na tayari unakuwa katika ibada. Ndani yake pia kuna kuweka nia ya kufunga kwa yule aliyesahau,” anasema.

Kwa mtazamo wake, daku si maandalizi ya kimwili pekee, bali ni daraja la kiroho linalomuingiza mja katika siku ya swaumu akiwa na utulivu, umakini na nia thabiti.

Kauli za madaktari

Mbali na msisitizo wa kidini, wataalamu wa afya wanasema daku ina mchango mkubwa katika kulinda afya ya mfungaji. Wakati wanazuoni wakizungumzia thawabu na baraka, madaktari wanathibitisha manufaa yake kisayansi.

Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni, Dk Mdhamini Francis, anasema kula daku husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu kwa muda mrefu, kudumisha nguvu na umakini, na kupunguza uchovu wa mapema.

“Daku ina faida nyingi kwa mfungaji ikiwamo kuweka sawa kiwango cha sukari, kudumisha nguvu na umakini. Mwili unahitaji nishati ili ubongo na misuli vifanye kazi vizuri. Bila kula kwa muda mrefu, mwili unaweza kuanza kutumia protini ya misuli kama chanzo cha nishati,” anasema.

Anaongeza kuwa kutokula kabisa hadi mchana kunaweza kuongeza tindikali tumboni na kusababisha maumivu, hivyo daku husaidia kupunguza hatari hiyo na kulinda misuli.

Naye mratibu wa huduma za lishe Wilaya ya Kilwa, Fahad Sabas, anasema daku ni kinga dhidi ya uchovu uliopitiliza, upungufu wa sukari mwilini, upungufu wa maji mwilini  na hata upungufu wa vitamini na madini.

Anashauri mfungaji kuchagua vyakula vyenye wanga usiokobolewa, protini kama maharage, kunde, njegere, mayai au maziwa, pamoja na matunda na mboga.

“Mchanganyiko huu husaidia sukari ya damu kupanda taratibu na kudumu kwa muda mrefu. Pia hupunguza hatari ya kula kupita kiasi wakati wa kufuturu, jambo linaloweza kuleta matatizo ya mmeng’enyo na ongezeko la uzito,” anasema.

Aidha, anasisitiza umuhimu wa kunywa maji ya kutosha wakati wa daku ili kusaidia mwili kuhimili muda wa kufunga bila kuathiri utendaji wa viungo.

Kwa upande wake, muumini wa Kiislamu, Mariam Abbas, anasema daku humwezesha kutimiza majukumu yake ya kila siku bila kuchoka.

“Mimi napendelea kula daku saa 10 usiku. Nikimaliza kula napumzika kidogo kisha naswali. Kunapokucha naendelea na majukumu ya kuwaandaa watoto kwenda shule na kazi za nyumbani bila kuchoka,” anasema.

Kwa ujumla, daku inabaki kuwa kiungo muhimu kati ya imani na afya. Ni ibada inayompa mfungaji nguvu za kimwili, uthabiti wa kiroho na maandalizi bora ya kukabiliana na siku ya swaumu.

Katika mafungamano hayo, daku inaendelea kuthibitisha kuwa ni zaidi ya mlo, kwani  ni nguzo muhimu ya mafanikio ya swaumu ya Ramadhani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *