Dar es Salaam. Kati ya wanamuziki wa mwanzo kabisa kutoka chini ya usimamizi wa Tanzania House (THT), ni Mwasiti (40), ambaye mwaka huu anatimiza miaka 20 tangu jina lake lilipoanza kuwa maarufu katika Bongofleva.
Mwasiti alitoka kupitia wimbo wake, Niambie (2006) uliotayarishwa katika studio binafsi ya Lady Jaydee, huku video yake ikisimamiwa na Director Adam Juma kutokea Visual Lab.
Niambie ni wimbo unaozungumzia urafiki wa kawaida kati ya mtu na mtu ambapo anataka kujua ipi sababu ya mizozo iliyozuka ghafla kati yake na rafiki yake, hivyo Mwasiti anataka kuambiwa kipi kibaya alichotenda.
Mwasiti alizaliwa Februari 2, 1986 katika hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam, na alianza kupenda muziki na hata kujihusisha nao tangu mwaka 1995 wakati huo akiwa na umri wa miaka tisa tu!
Alipata elimu ya msingi Mwenge alipohitimu mwaka 1999, kisha sekondari akasoma Mbezi Beach ambako ndio hasa ndoto yake ya muziki iliiva akianzisha klabu ya muziki shuleni hapo kabla ya kuhitimu 2003.
Mwaka uliofuatia akajitosa katika shindano na kusaka vipaji vya uimbaji la Coca-Cola Popstar 2004 ambapo alivuka mchujo wa kwanza ila akashindwa kushiriki awamu iliyofuatia baada ya mzazi wake kumkataza.
Ikumbukwe Coca-Cola Popstar 2004, washindi watatu kutokea Tanzania walikuwa ni Shaa, Witnesz ‘Kibonge Mwepesi’ na marehemu Langa. Hawa walikuja kuunda kundi la Wakilisha, huku Kenya kukiwa ni kundi la Sema na Uganda, Blu 3.
Waimbaji wa kike Bongo waliomvutia zaidi Mwasiti ni Lady Jaydee na Ray C ambao wakati huo walikuwa wakitamba sana, hivyo alitamani siku moja naye awe kama wao.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, ndipo rafiki yake mmoja akampeleka THT kuonyesha kipaji chake, ni kama tayari Mwasiti alipangiwa kuwapo hapo maana alipofanyiwa majaribio machache tu, yote alifaulu.
Wakati huo alikuwa akiimba miondoko ya RnB ila aliyekuwa msimamizi wa THT, marehemu Ruge Mutahaba akamtaka kubadilika na kuimba Afropop na Afrofusion akiamini huo ndio muziki unaoweza kumfikisha mbali.
Kuanzia hapo kilichofuata ni historia, akitoka na wimbo wake, Niambie (2006) uliopokewa vizuri na kumfanya kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2007.
Alikuja kufanya vizuri zaidi na wimbo wake, Hao (2007) aliomshirikisha rapa Chid Benzi, huu ulitayarishwa na Lamar ambaye amefanya kazi na Bongo Records, 41 Records hadi kuja kufungua studio yake, Fishcrub.
Professor Jay ndiye alitakiwa kusikika katika wimbo huo, lakini alikuwa amesafiri nje ya nchi, Mwasiti alimsubiri kwa muda na baadaye akashauriana na Ruge kuwa nafasi hiyo apewe Chid Benzi.
Kwa mujibu wa Mwasiti, siku ya kurekodi Chid alikuja studio wakati mvua kubwa sana ikinyesha, akaomba apewe kalamu nyekundu ili aandike vesi yake, na ndani ya muda mfupi akawa amemaliza na kurekodi.
Hata hivyo, Ruge hakuukubali sana wimbo huo pindi alipousikia, hivyo ulichelewa kidogo kutoka, lakini ulipoachiwa tu ukapokewa vizuri na hadi sasa Chid anautaja kama kolabo yake kali zaidi kwa muda wote.
Mwasiti alikuja kufunika zaidi na wimbo wake mwingine, Nalivua Pendo (2008) uliotayarishwa MJ Records, na huu nao ulimpatia tuzo ya TMA ukishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Zouk 2009.
Ni wimbo ulioandikwa na Mzee Abuu kutokea Kariakoo kisha akauuza kwa Ruge ambaye kwa mara ya kwanza alimpa marehemu Maunda Zorro aurekodi, lakini akaona hajautendea haki ndipo akatoa kwa Mwasiti.
Hata hivyo, huwezi kuzungumzia ukubwa wa Mwasiti bila kutaja kolabo yake na Quick Rocka, mwanachama wa zamani wa kundi la Rockaz, akiwa na wenzake kama Chief Rocka, Dau Rocka na Mo Rocka.
Wawili hao walitoa wimbo maarufu hadi sasa, Sio Kisa Pombe (2010) ambao sehemu ya Mwasiti aliandikiwa na Barnaba ambaye yeye ni mtu wa mwanzo kuona kuwa anafaa kujiunga na THT.
Kufanya vizuri kwa wimbo huo na ule aliomshirikisha Chid Benzi (Hao), kulimpa Mwasiti nguvu ya kuendelea na wasanii wa Hip Hop akifanya kolabo na Godzilla (Soldier & Leo), Billnass (Bado) na Roma (Fall in Love).
Na wasanii wa Hip Hop waliowahi kumshirikisha yeye Mwasiti katika ngoma zao ni D Knob (Nishike Mkono), Lord Eyes (Kwanini), Izzo Bizness (Walala Hoi), Godzilla (First Class & Genius) n.k.
Mwaka 2013, Mwasiti aliweka rekodi ya kuwa msaniii wa kwanza wa kike Bongo kutajwa kuwania vipengele vitano katika tuzo za TMA, lakini kwa bahati mbaya hakushinda hata moja!
Aliwania Msanii Bora wa Kike, Msanii Bora wa Kike Bongofleva, Wimbo Bora wa Kushirikiana (Mapito ft. Ally Nipishe), Wimbo Bora wa Zouk/Rhumba (Mapito) na Wimbo Bora wa Mwaka (Mapito).
Hadi sasa akiwa ameshinda tuzo, ametoa albamu moja (Kamili) na EP moja (The Black Butterfly), Mwasiti anaendelea kufanya muziki wake ila hasa akijikita katika miradi ya kijamii inayowalenga wanawake na watoto.