
Nchini DRC, lori la MSF lililobeba vifaa vya matibabu limeshambuliwa mnamo Februari 18, 2026, na watu wenye silaha. Shambulio hilo lilitokea Mayi ya Moto, katika eneo la Rutshuru (mashariki mwa DRC), eneo linalodhibitiwa na AFC/M23. Lori hilo lilikuwa njiani kuelekea eneo la afya la Kibirizi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na vyanzo vya ndani vilivyowasiliana na RFI, inaonekana kuwa shambulio hilo lilikuwa la kuvizia ambalo pia lililenga gari lingine lisilo la kiserikali na watu binafsi waliokuwa wakisafiri katika barabara hiyo.
Katika hatua hii, ni vigumu kubaini wahusika wa shambulio hili mashariki mwa DRC. Eneo hilo hapo awali lilikuwa likidhibitiwa na kundi la waasi wa Kihutu wa Rwanda (FDLR), lililoundwa awali na wahalifu wa zamani wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, kabla ya kuanguka chini ya udhibiti wa kundi la kisiasa na kijeshi la AFC/M23.
Kulingana na RFI, takriban wanaume kumi wakiwa wamevaa nguo za kiraia—lakini wakiwa na silaha—wakiwa wamesimama pande zote mbili za barabara, walifanya shambulio hilo mnamo Februari 18 saa sita mchana. Shambulio hilo lililenga lori la shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), gari la Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC), na pikipiki kadhaa za kukodiwa.
Waliokuwa ndani ya lori la MSF walitishiwa vikali na kulazimishwa kupiga magoti, huku bunduki na mapanga zikiwaelekezea. Dereva wa MSF alijeruhiwa. Kulingana na taarifa zetu, gari la NRC lilipakuliwa vifaa vyake muhimu vilivyokusudiwa kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo. Hata hivyo, madereva wa pikipiki za kukodiwa na raia wengine walipigwa, kuibiwa, na kuvuliwa nguo.
Mwaka wa 2025, matukio 626 yaliathiri wafanyakazi wa mashirka ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini DRC
Shambulio hili la hivi karibuni linakuja huku ufikiaji wa kibinadamu katika eneo hilo ukibaki mdogo sana, huku mapigano yakiendelea kurindima na watu wakikimbia makazi yao.
Mwaka jana, OCHA, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, ilirekodi matukio 626 yaliyoathiri wafanyakazi wa mashirka ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini DRC. Mnamo Desemba pekee, matukio 48 yalirekodiwa, nusu yake yakirekodiwa katika mkoa wa Kivu Kusini. Mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri ilifuata.