Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa hajaridhishwa na uandikishwaji wa watu walioko kwenye makundi maalumu kwenye mpango wa bima ya afya kwa wote na kuagiza waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) kushirikishwa ili wawasaidie kuwatambua wahusika kwa urahisi.

Mkoa wa Dodoma ulikuwa umepanga kuandikisha jumla ya wanachama 46,000 lakini mpaka sasa wameandikisha asilimia 30 pekee huku changamoto ikitajwa kuwa ni mwitikio mdogo wa wananchi pamoja na uchache wa vifaa vya kuwaandikishia.

Senyamule ameyasema hayo leo Februari 20, 2026 kwenye kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe jijini Dodoma na kuagiza hatua zaidi zichukuliwe ili wote wanaostahili kuandikishwa wafikiwe kwa wakati.

Amesema ni aibu kwa mkoa wa Dodoma kutowafikia walengwa wa mpango wa bima ya afya kwa wote kwa muda uliopangwa na Serikali na na wakati wanajulikana na hivyo ameagiza waratibu wa Tasaf kushirikishwa kwenye mpango huo kwa kuwa wanawafahamu walengwa wote na mahali wanapopatikana.

“Ni aibu kwa mkoa wote wa Dodoma kuandikisha asilimia 30 tu ya walengwa wa mpango wa bima ya afya kwa wote na wakati walengwa wanajulikana, tatizo ni nini? Hivi hawa waratibu wa Tasaf wenye watu wao wanashirikishwa kweli? Washirikisheni kuwatambua wawasaidie mbinu wanazotumia kuwakusanya ndani ya siku mbili wanapokuwa na jambo lao ili tufikie lengo,” amesema Senyamule.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa mpaka sasa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeandikisha asilimia 42 ya walengwa, Bahi (34), Chamwino (32), Mpwapwa (30), Chemba (30), Kongwa (29), Kondoa Mji (26) na halmashauri ya Kondoa asilimia 21.

Amesema walengwa kwenye mpango huu wa kwanza ni wale ambao hawana uwezo kwa kugharamia bima ya afya na hii ni fursa kwao kupata matibabu bure, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuwafikia ili wote waandikishwe na hatua itakayofuata ni ile ya kuwahamasisha wananchi kulipia Sh150,000 kwa kaya.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Thomas Rutachunzibwa amesema uandikishaji wa walengwa wa awamu ya kwanza umekumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo wahusika kutokuwa na uelewa wa uandikishaji huo na uchache wa mashine za kuwaandikisha.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni walengwa kwenda shuleni huku uandikishaji huo ukihitaji kaya nzima kuwepo wakati wa uandikishaji lakini wategemezi wengi ni wanafunzi, hivyo kuna baadhi ya maeneo wamelazimika kuwaombea ruhusa shuleni ili waweze kuandikishwa kwenye bima ya afya kwa wote.

“Lakini kama unavyofahamu huu ni msimu wa kilimo, wahusika wengi wakifuatwa wanakuwa mashambani na wanashinda huko hivyo wanakosa muda wa kujiandikisha, lakini tumepokea malekezo yako ya kuwashirikisha waratibu wa mfuko wa Tasaf ili waweze kuwakusanya na wapate haki yao ya kupata bima ya afya kama maelekezo ya serikali yanavyotaka,” amesema Dk Rutachinzibwa.

Naye mwakilishi wa Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Dodoma, Irene Kataraia amesema jumla ya walengwa 46,000 wanatakiwa kuandikishwa kwenye awamu hii ya kwanza japo kuna changamoto mbalimbali zilizojitokeza kutofikia lengo, ikiwemo uchache wa vifaa na wataalamu wa kutumia BVR kwa ajili ya kuwaandikisha.

Amesema lakini tatizo hilo limeshatatuliwa na vifaa vimeongezwa hivyo idadi ya kuandikisha walengwa itaongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.

Mpango wa bima ya afya kwa wote umeanza kutumika hapa nchini tangu Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alipoitangaza Januari 26, 2026 ‎ambapo tangu wakati huo makundi maalumu yameshaanza kuandikishwa kwenye mpango huo kwa kutumia mamlaka za utambuzi.

‎Aidha kwa mujibu wa mamlaka za utambuzi nchini kuna asilimia 26.4 ya kaya ambazo hazina uwezo zenye jumla ya watu 3,917,000 ambao watapewa huduma ya bima ya afya kwa wote kwa awamu ya kwanza, ambao hawana uwezo wa kulipia.
Makundi hayo ni ya wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, watu wenye ulemavu na wazee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *