Tanga. Mbunge wa Jimbo la Tanga, Kassim Amar Mbaraka amewataka wakazi wa Jiji la Tanga kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Akizungumza Jumamosi, Februari 21, 2026, wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa wataalamu wasio na uzoefu kuhusu matumizi ya dawa za kulevya watakaosaidia waraibu kuacha matumizi hayo, mbunge huyo ameonya kuwa endapo hatua hazitachukuliwa mapema, athari za tatizo hilo zitakuwa kubwa si kwa jiji hilo tu bali kwa taifa kwa ujumla.

Amesema taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya wauza dawa hizo wanafahamika katika jamii wanamoishi, lakini hawaripotiwi kwa vyombo vya dola, hali inayochangia kuendelea kwa biashara hiyo.

“Mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi. Wapo wanaowajua wahusika lakini wananyamaza. Tukikaa kimya, tunaliangamiza taifa letu,” amesema.

Mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, akieleza kuwa sambamba na hatua za kisheria, juhudi za kuwasaidia waraibu kurejea katika maisha ya kawaida ni sehemu muhimu ya mapambano hayo.

“Madhara ya dawa za kulevya yanaonekana wazi. Vijana wetu, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa, wanaangamia. Hatupaswi kuoneana huruma katika suala hili. Tuwafichue popote walipo,” alisema Mbaraka.

Mafunzo hayo yanaratibiwa na Colombo Plan kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kupitia Mradi wa Programu ya Tanga Yetu, yakitekelezwa na asasi ya kiraia ya Gift of Hope.

Kwa upande wake, Mratibu wa Gift of Hope, Said Bandawe, amesema mamlaka zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti uingizwaji wa heroini, huku juhudi sasa zikielekezwa katika kudhibiti dawa nyingine zinazopatikana kirahisi mitaani.

Ameonya kuwa biashara ya dawa za kulevya ni kosa la jinai lenye adhabu kuanzia miaka 30 jela hadi kifungo cha maisha, akihimiza Watanzania kujikita katika shughuli halali za kiuchumi badala ya kuharibu maisha ya vijana.

Bandawe, ambaye aliwahi kuwa mraibu kwa zaidi ya miaka 22 kabla ya kupona, amesema zaidi ya watu 1,000 wanapatiwa huduma ya methadone mkoani Tanga.

Amebainisha kuwa huduma ya methadone sasa itaanza kupatikana wilayani Muheza, hatua inayopunguza adha kwa waraibu waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo.

“Tiba imeleta mabadiliko makubwa. Wapo waliokuwa waraibu, leo ni viongozi na waelimishaji katika jamii zao. Hii inaonyesha vita hii inawezekana kushinda,” alisema Bandawe.

Akizungumzia uzoefu wake binafsi, amesema aliathiriwa na makundi rika na mazingira ya upweke, lakini sasa ametimiza miaka 12 bila kurejea matumizi ya dawa za kulevya, akitumia maisha yake kuwahudumia wengine kama sehemu ya safari yake ya uponyaji.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Kliniki ya Methadone Kihonda, Mussa Kilasa, amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuboresha mbinu za kuwahudumia waraibu na kutoa elimu ya kinga kwa vijana walioko kwenye mazingira hatarishi.

Naye Elizabeth Mtenga, mwelimishaji rika kutoka Gift of Hope, amesema wamejengewa uwezo wa kutumia lugha sahihi wanapotoa elimu ili kuepuka unyanyapaa kwa waraibu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi wa mapambano hayo.

Takwimu zinaonyesha Mkoa wa Tanga unashika nafasi ya pili kwa matumizi ya dawa za kulevya nchini baada ya Dar es Salaam, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wadau na jamii kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *