
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, makumi ya watu wameuawa kufuatia mashambulio dhidi ya vituo vya afya nchini Sudan.
Hayo yameelezwa na Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X na kubainisha kwamba, katika siku 50 za kwanza za mwaka huu wa 2026, mashambulizi matano dhidi ya vituo vya afya tayari yalikuwa yamerekodiwa nchini Sudan, ambayo yaliwauwa watu 69 na kujeruhi wengine 49.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameeleza kuwa, Jumapili iliyopita, hospitali moja ililengwa kusini mashariki mwa jimbo la Sennar, na kuwauwa wagonjwa watatu na kuwajeruhi watu wengine saba ikiwa ni pamoja na mfanyakazi mmoja.
WHO pia imethibitisha takriban mashambulizi 206 dhidi ya vituo vya afya tangu kuanza mapigano hayo mnamo Aprili mwaka 2023, ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 2000 na kujeruhiwa mamia ya wengine.
Shirika la Afya Duniani (WHO) tarehe 10 mwezi huu lilitahadharisha pia kuwa mfumo wa afya wa Sudan unakabiliwa na mashambulizi baada ya vituo vitatu vya afya katika jimbo la Kordofan Kusini kushambuliwa mwanzoni mwa mwezi huu.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti yake kwamba, ukatili uliofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) wakati wa kuutwaa mji wa El-Fasher huko Darfur Magharibi nchini Sudan mwezi Oktoba mwaka jana, una “alama za mauaji ya kimbari” dhidi ya jamii za Zaghawa na Fur.