KOCHA wa Yanga, Pedro Gonçalves amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo kuhusu kiungo Pacôme Zouzoua akisema maumivu yake siyo makubwa sana na anaweza kuwa sawa hivi karibuni.

Pacome alicheza kwa dakika 40 na kuingia Mudathir Yahya katika mechi ya mwisho ya kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie iliyochezwa wikiendi iliyopita mjini Zanzibar, baada ya kugongana na mchezaji wa wapinzani hao tukio lililomfanya atolewe mapema kutokana na kushindwa kuendelea.

Tangu hapo mchezaji huyo alikosekana katika mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo Yanga iliifunga Cosmopolitan kwa mabao 2-0, huku pia akitarajiwa kukosekana leo dhidi ya Namungo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema madaktari wanapambana kuhakikisha Pacome anakuwa sawa ili arudi uwanjani.

Alibainisha kuwa, wamempa mapumziko ya kuhakikisha anapona vizuri kabisa kwani kama wakiendelea kumtumia hivi sasa huenda akaumia zaidi na kufanya jeraha kuwa kubwa.

“Pacome anaendelea vyema kwa sasa. Tumempa mapumziko kidogo ili aweze kuwa sawa zaidi, kwani yeye ni miongoni mwa viungo muhimu kwenye kikosi hiki, kwa hiyo kuendelea kumtumia wakati hayuko sawa ni kama kuendelea kumuumiza zaidi.

“Madaktari wanaendelea kupambana ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na ni imani yangu kwamba hatakaa nje kwa muda mrefu. Huenda akarejea uwanjani hivi karibuni kwani hali yake si mbaya,” alisema Pedro.

Kwa mujibu wa matabibu wa Yanga, Pacome huenda akaiwahi Kariakoo Dabi, mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Machi Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo Yanga itaikaribisha Simba kuanzia saa 2:15 usiku.

Pacome ambaye alifunga bao pekee katika Kariakoo Dabi iliyopita ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Simba, msimu huu katika ligi amefunga mabao matatu akicheza mechi tano kwa dakika 341.

MZIZE JERAHA JINGINE

Mzize hakuonekana uwanjani tangu msimu uanze, akisumbuliwa na jeraha la goti lililomsumbua tangu mwaka jana. Alirudi na kucheza mechi moja ya hatua ya makundi, lakini taarifa mbaya ni kwamba amepata jeraha jingine tofauti.

Kocha anasema kuwa Mzize amepata tatizo jingine, si lile lile, na wanachosubiri ni ripoti ya daktari ili waweze kujua tatizo hasa ni nini.

“Kuhusu Mzize, amepata maumivu tena. Si kwa tatizo lile lile, ni jingine, lakini pia madaktari wanapambana kuhakikisha anakuwa sawa. Jambo la muhimu ni kumuombea asiwe na jeraha kubwa litakalomfanya akae nje tena.”

Akaongeza: “Nimewaambia wachezaji hawatakiwi kujiona wakosaji baada ya kutolewa katika michuano ya CAF. Wanachotakiwa ni kuendelea kupigania malengo yao mengine yaliyosalia. Walipambana sana, lakini tofauti ndogo imewaangusha na kuwatoa.”

Ikumbukwe kuwa Yanga ilitolewa wikiendi iliyopita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni timu ya nne kutoka Ligi Kuu Bara, ikianza Simba, Singida Black Stars, Azam FC na Yanga kwa msimu ambao Tanzania iliandika rekodi mpya kwa kuingiza timu nne katika michuano ya CAF.

Mzize alitokea benchi katika mchezo dhidi ya FAR Rabat ya Morocco, ambapo alicheza kwa dakika 10 bila kufunga wala kutoa asisti, huku Yanga ikipoteza kwa bao 1-0 ugenini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *