
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kuhusu uchukuaji hatua za kujibu mapigo kukabiliana na uamuzi haramu wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, EU wa kuviwekea lebo ya ugaidi baadhi ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, matini ya taarifa hiyo, ambayo ilitolewa jana Jumamosi, Februari 21, 2026, inaeleza kama ifuatavyo: Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imetoa jibu kwa uamuzi haramu na usio na msingi uliochukuliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya mnamo Februari 19, 2026, kwa kutangaza ifuatavyo: Kwa kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, kinyume na misingi na sheria kuu za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa zimelitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC ambalo kinatambuliwa kama moja ya nguzo za vikosi rasmi vya ulinzi vya nchi kuwa ni shirika la kigaidi, Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia msingi wa uchukuaji hatua ya kujibu mapigo kwa kutumia Kifungu cha 7 cha sheria ya “Uchukuaji Hatua Mkabala Dhidi ya Kutangazwa na Marekani Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama Shirika la Kigaidi na Marekani” iliyoidhinishwa mwaka 2019, ambayo inabainisha kwamba “nchi zote ambazo kwa namna yoyote ile zinafuata au kuunga mkono uamuzi wa Marekani wa kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni shirika la kigaidi zitahusishwa katika uchukuaji ya kujibu mapigo”, inayatangaza Majeshi ya Wanamaji na Majeshi ya Wanaanga ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwa yanajumuishwa kwenye kanuni hiyo iliyotajwa na vifungu vyake, pamoja na vifungu vyake kikiwemo Kifungu cha 4, na kwa muktadha huo, kwa kutumia msingi wa uchukuaji mkabala, inayatambua na kuyatangaza majeshi hayo kuwa ni mashirika ya kigaidi…/