Sambamba na kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, jeshi la utawala wa Kizayuni limeshadidisha mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi huko Palestina.

Vyombo vya habari vimeripoti kwamba, uvamizi mkubwa uliofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi. Ripoti zinaonyesha kuwa, kwa kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, mashambulizi ya jeshi la utawala huo wa kivamizi pia yameongezeka.

Vyanzo vya ndani viliripoti jana kwamba, katika uvamizi wao dhidi ya mji wa al-Khalil vikosi vya utawala vamizi wa Israel, vilishambulia mji wa Surif kaskazini mwa al-Khaliil, mji wa Awa magharibi mwa al-Khalil, na mji wa Deir Samet magharibi mwa Dura kusini mwa mji huo. Kulingana na ripoti zilizochapishwa, vikosi vilivyovamia viliteka magari kadhaa katika uvamizi dhidi ya al-Khalil.

Mji wa Nablus, kama maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi nao ulishuhudia mashambulio ya wanajeshi wa Israel. Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanajeshi wa utawala huo ghasibu pia walishambulia mji wa “Qasra” kusini mwa Nablus.

Jeshi la Kizayuni pia lilishambulia Beit Laham huku likishambulia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi. Katika shambulio hilo dhidi ya mji wa Al-Obeidiyah, mashariki mwa Beit Laham, wanajeshi wa Israel walifyatua gesi ya kutoa machozi kwa raia na maduka.

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba, mipango ya utawala ghasibu wa Israel ya kuimarisha udhibiti wa sehemu za Ukingo wa Magharibi inakwenda sambamba na kutwaa eneo hilo kimabavu.

Wakati huo huo, zaidi ya nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimelaani mpango wa Israel wa kupora na kuyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, na kuyatambua maeneo hayo ya Palestina kama “milki ya serikali” ya Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *