Iran imejiunga na nchi na mashirika kadhaa ya Kiislamu na Kiarabu katika kulaani vikali kauli za balozi wa Marekani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, aliyedokeza kuwa Israel ina haki ya kupanua uvamizi wake hadi sehemu kubwa ya Asia Magharibi.

Taarifa hiyo imejiri baada ya Mike Huckabee balozi wa Marekani katika utawala haramu wa Israel kusema katika mahojiano kuwa ingekuwa “sawa kabisa” iwapo Israel ingenyakua ardhi yote kati ya Mto Nile nchini Misri na Mto Frati katika ardhi za Syria na Iraq.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema matamshi ya Huckabee ni “uthibitisho wa wazi wa ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani katika vita vya uchokozi vya upanuzi wa utawala wa Israel, pamoja na mauaji ya kikoloni dhidi ya Wapalestina.”

Aidha, alionya kuwa “kauli zenye  itikadi kali” za balozi huyo wa Marekani zitazidi kuutia moyo utawala unaonyakua ardhi kuendelea na “uhalifu wa kikatili na hatua zisizo halali dhidi ya Wapalestina, sambamba na uchokozi wake wa mara kwa mara dhidi ya mataifa ya eneo hili.”

Nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu za eneo hilo yamekosolewa na kulaaniwa vikali na nchi hizo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC, Jumuiya ya Waarabu na makundi ya ukombozi wa Palestina.

Huckabee alitoa matamshi hayo wakati wa mahojiano na mchambuzi wa habari wa Marekani Tucker Carlson, yaliyotangazwa siku ya Ijumaa, alipokuwa akitilia mkazo suala la mipaka ya kijiografia ya utawala wa kizayuni.

Eneo hilo alilopendekeza balozi wa huyo wa Marekani ni Lebanon ya sasa, Syria, Jordan na sehemu kadhaa za Saudi Arabia.

Matamshi aliyotoa Huckabee siku ya Ijumaa yameibua mjibizo wa haraka wa kukosoa na kulaani kutoka nchi za Misri na Jordan, Saudi Arabia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC, Jumuiya ya Waarabu na makundi ya ukombozi wa Palestina.

 Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imelaani matamshi ya balozi wa US katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel ikisema yanaakisi mawazo ya kikoloni na kuonyesha jinsi Washington inavyoafikiana na miradi ya “udhibti na uunganishaji wa ardhi unaofanywa na utawala wa Kizayuni”.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema matamshi ya Mike Huckabee ni “mfano dhahiri wa mawazo ya kikoloni ambao ndio msingi wa kuasisiwa vuguvugu la Kizayuni.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *