Dar es Salaam. Wakati Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ikiongezewa muda wa siku 42, wadau wamekuwa na mitizamo tofauti huku wakidokeza inaweza kupoteza imani kwa wananchi.

Tume hiyo iliyoteuliwa na kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Othuman Chande ilipewa siku 90 kukamilisha kazi yake kuanzia Novemba 20, 2025 hadi Februari 20, 2026.

Kwa nyongeza hiyo ya muda, tume sasa inapaswa kukamilisha kazi na kuwasilisha taarifa yake kabla au ifikapo Aprili 3, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Februari 21, 2026 na tume hiyo, nyongeza ya siku 42 imetolewa ili kuipa muda wa kukamilisha uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Taarifa hiyo pia inasema muda huo utasaidia kutoa fursa ya kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo nchini au nje ya nchi, kuwasiliana na Tume ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu au taasisi itakayokosa nafasi ya kusikilizwa.

Sababu nyingine za kuongeza muda zimetajwa ni wingi na mchanganyiko wa taarifa zilizokusanywa na zinazoendelea kukusanywa, hivyo tume inahitaji muda zaidi wa kufanyia uchambuzi wa kina.

Nyingini kwamba, tume inalazimika kutumia wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi wenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kisayansi na uchambuzi wa kidijitali wa baadhi ya taarifa na vielelezo kutokana na aina ya matukio na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, na unaoendelea kuwasilishwa.

Sababu nyingine ni tume kubaini mapengo kadhaa katika taarifa na vielelezo vilivyokusanywa hadi sasa, hivyo kuhitaji kutafuta au kupata taarifa zaidi ili kukamilisha ushahidi kwa kila hoja inayohusika kutoa fursa kwa wadau wachache muhimu ambao kwa sababu mbalimbali bado hawajafika mbele ya tume licha ya kupelekewa mialiko zaidi ya mara moja.

Taarifa hiyo imewataja wadau hao ni baadhi ya viongozi wa dini, wa vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi.

Pia, imeeleza wingi wa wananchi wanaoendelea kufika mbele ya tume kuwasilisha taarifa, ushahidi na ushauri wao ni miongoni mwa sababu za kuongezwa muda huo.

Kutokana na fursa hiyo ya tume kuongezewa muda, Mwenyekiti wake Jaji Othuman Chande ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwasilisha ushahidi kwenye tume kwa kutumia njia zote zilizokuwa zimeainishwa awali.

Njia hizo ni majadiliano ya ana kwa ana, mawasilisho ya maandishi kwa njia ya posta au tovuti maalumu ya tume, barua pepe, ujumbe mfupi wa simu, kujaza dodoso maalumu kwenye mtandao (www.tume.uchunguzi.go.tz) au kupitia mitandao mingine ya kijamii.

Pia, tume hiyo imesema baadhi ya viongozi wa dini, wa vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi ambao wamepewa mialiko na tume lakini bado hawajafika mbele ya tume,  watumie fursa hiyo kufika au kuwasiliana na tume kutoa mchango wao katika uchunguzi unaoendelea kwa manufaa ya wananchi, wadau na nchi kwa jumla.

Taarifa hiyo pia imewataka Watanzania kuendelea kuipa tume ushirikiano ili kuiwezesha kukamilisha kazi yake ya uchunguzi.

Aidha, tume hiyo imeeleza kuwa, itaendelea kufanya vikao vya wazi isipokuwa pale mashahidi kwa faida ya usalama wao hawatapenda majina yao, sura na taarifa zao zitolewe kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

Mwananchi imezungumza na wadau mbalimbali juu ya muda huo ulioongezwa.

Wadau hao wamesema kuongezwa muda ni jambo la kawaida huku wakihofia siku 42 ni nyingi kwa kuzingatia uzito wa jambo na uhitaji wa wananchi kujua nini kilitokea ili kuondokana na hali iliyotokea isijirudie.

Mhadhiri wa zamani wa mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amesema kukaa siku nyingi bila kutolewa taarifa hiyo kunaweza kuathiri imani na matumaini ya wananchi kuhusu uchunguzi unaofanyika.

“Kama wameomba na mheshimiwa Rais ameona hekima ya kuwaongezea muda ni jambo jema, lakini kutokana na unyeti wa jambo, tume inatakiwa kufanya kazi kwa weledi ndani ya muda wanaopewa kwani, kuzidi kuongeza muda kunaweza kuathiri imani ya jamii kwao.

“Siku 90 walizopewa hazikuwa chache, na katika utafiti hauwezi kuyafikia makundi yote, unatumia sampuli. Najua wanasekretarieti inayofanya kazi, hivyo wangejitahidi wamalize na kutoa ripoti mapema ili jamii ijue walichobaini kwenye uchunguzi wao,” amesema.

Kwa mtazamo wa kisheria, Wakili Dk Onesmo Kyauke amesema ni jambo la kawaida kuongeza muda hasa ikiwa zipo sababu za msingi za kufanya hivyo.

“Hata mahakamani, mnaweza mkakaa kusubiri hata jambo limeisha lakini hakimu anatakiwa kuandika ripoti anaweza kupewa muda mkasubiri.

“Mimi naona jamii iwape muda wamalizie, watoe hiyo ripoti jamii ijue walichokutana nacho kwenye uchunguzi,” amesema.

Mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, Frank Charles yeye amesema siku 90 zilikuwa nyingi, “kuongezewa zingine 42 zinafanya uchunguzi kukaa muda mrefu hadi tutasahau sasa. Ilipaswa ripoti itoke mapema lakini kusogeza mbele inatutia wasiwasi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *