KIKOSI cha Simba usiku wa jana kilikuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kumalizana na wenyeji wao, Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku mastaa wanne wa timu hiyo wakibeba matumaini kabla ya kuifuata Yanga katika pambano la Dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu kwa msimu huu itakayopigwa Zanzibar.

Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kumalizana na TZ Prisons iliyopeleka pambano hilo Jamhuri baada ya Uwanja wa Sokoine Mbeya inaoutumia kufunguliwa siku chache tangu ulipofungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baada ya mechi hiyo inajianda kucheza tena keshokutwa Jumatano dhidi ya Dodoma Jiji.

Mara baada ya viporo hivyo viwili kumalizika, Simba itavuka Bahari ya Hindi kuifuata Yanga katika mechi ya dabi, lakini ikiwa na mzuka kutokana na wachezaji wanne waliopo kikosi kwa sasa kubeba matumaini ya kikosi hicho kinachosaka ushindi wa kwanza kwa Yanga tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-0 Aprili 16, 2023 katika Ligi Kuu.

Wachezaji waliobeba tumaini ya Simba kwa sasa katika dabi ni; Libasse Gueye aliyesajiliwa dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, sawa na Alain Anicet Oura raia wa Ivory Coast, aliyejiunga nao, baada ya kuachana na IF Gnistan ya Jiji la Helsinki, Finland.

Tangu ajiunge na timu hiyo katika dirisha dogo, Gueye amecheza dakika 467 katika mashindano yote na kati ya hizo, amefunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, akionyesha kiwango kizuri chenye kuvutia kwa muda mfupi kikosini.

Kwa upande wa Oura, amecheza dakika 482, katika mashindano yote na kati ya hizo amechangia mabao matatu, baada ya kufunga mawili ambayo ni ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kuasisti lingine moja pia, kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Nyota mwingine aliyebeba tumaini ni Mzambia Clatous Chama aliyerejea tena Msimbazi kwa mara ya tatu msimu huu, baada ya awali kutimkia kwa watani zao wa jadi Yanga na baadae kujiunga na Singida Black Stars aliyoachana nayo.

Chama amechangia bao moja tu la Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, wakati timu hiyo ilipotoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia, iliyopigwa Februari 1, 2026, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kipa, Mahamadou Tanja Kassali, aliyejiunga pia na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026, akitokea AS FAN Niamey ya kwao Niger, ni miongoni mwa nyota walioonyesha kiwango kizuri, baada ya kutoruhusu bao (Clean Sheets), katika mechi mbili.

Kassali, amejiunga na timu hiyo baada ya kuumia kwa kipa mwenzake, Moussa Camara, ambaye hadi sasa amecheza mechi tano katika mashindano yote, akiwa ndiye tegemeo kikosini humo, baada ya awali pia, Yakoub Suleiman aliye majeruhi.

Simba na Yanga zitakutana katika pambano hilo la 115 katika Ligi ya Bara tangu 1965, huku vijana wa Jangwani wakiwa wenyeji na rekodi na kushinda mechi sita mfululizo za mashindano yote katika dabi ya Kariakoo, lakini ikishikilia ubingwa wa Ligi kwa msimu wa nne mfululizo mbele ya Wekundu wa Msimbazi.

Tayari makocha wa timu zote, Pedro Goncalves wa Yanga na Steve Barker wa Simba wamesema akili zao kwa sasa zipo katika mechi za viporo kabla ya kuanza kuifikiria Dabi itakayopigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.

Hilo ni pambano la kwanza la Ligi kwa timu hizo kukutana tangu zilipokutana mwaka 1992 katika michuano ya Kombe la Kagame na Simba kushindwa kwa penalti baada ya sare ya 1-1 katika dakika 120.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *