
Mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, Steve Witkoff, amesema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameonyesha mshangao mkubwa kuhusu sababu zinazofanya Iran isikubali masharti ya Washington katika mazungumzo yanayohusu mpango wake wa nyuklia.
Akizungumza katika mahojiano na Lara Trump kwenye kituo cha Fox News, Witkoff amesema kuwa Trump alionekana kukerwa na msimamo imara wa Iran wa kutosalimu amri. Witkoff alidokeza wazi kuwa Trump alidhani Iran inapaswa kulegeza msimamo wake kutokana na shinikizo kubwa linaloikabili.
Witkoff amesema: “Rais anaelewa kuwa ana chaguo nyingi mezani lakini ana shauku ya kujua kwa nini, chini ya shinikizo hili lote la kijeshi, hasa uwepo mkubwa wa meli za kivita na nguvu za baharini, Iran haijasema wazi: hatutaki silaha ya nyuklia, na haya ndiyo tuko tayari kufanya.”
Witkoff alidai kuwa Iran imeongeza kiwango cha urutubishaji wa urani zaidi ya mahitaji ya matumizi ya kiraia, akisisitiza kuwa mstari mwekundu wa Trump unabaki kuwa urutubishaji sifuri wa urani.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia, ikiwa ni pamoja na urutubishaji urani ni kwa ajili ya malengo ya amani kama hasa kuzalisha nishati na pia kwa ajili ya sekta za tiba, kilimo na viwanda.
Katika mahojiano hayo, mjumbe huyo wa Marekani pia alithibitisha kuwa amekutana na Reza Pahlavi, mwana wa mfalme katili wa zamani wa Iran, akisema mkutano huo ulifanyika “kwa maelekezo ya rais,” bila kufafanua zaidi juu ya maudhui yake.
Kauli hizi zinakuja wakati mvutano kati ya Tehran na Washington ukiendelea kuongezeka. Kwa upande mmoja, Trump anaendelea kuitaka Iran “kuafiki makubaliano,” lakini kwa upande mwingine, Marekani imekuwa ikiongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Hindi, jambo linalozua wasiwasi mkubwa miongoni mwa mataifa ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa haitaanzisha vita, lakini itajibu kwa nguvu hujuma yoyote ya kijeshi inayolenga mamlaka na usalama wake. Tehran imekumbusha kuwa mashambulizi ya Israel Marekani mwezi Juni mwaka jana yalisababisha Iran kujibu kwa makombora ya balistiki dhidi ya ngome za utawala wa Israel na kituo cha anga cha Al Udeid nchini Qatar, ambacho ni ngome muhimu zaidi ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.