
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) itafanya mkutano wa dharura katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje Alhamisi ijayo kujadili maamuzi ya hivi karibuni ya Israel yanayozidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na unyakuzi wa ardhi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi.
Jumuiya hiyo imesema katika taarifa iliyotolewa na Sekretarieti yake Kuu kwamba mkutano huo umeitishwa kwa ombi la Mamlaka ya Ndani ya Palestina, kwa lengo la kuratibu misimamo na kujadili hatua za pamoja ili kukabiliana na sera za Israel zinazolenga kubadilisha hali ya kisheria, kisiasa na idadi ya watu ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, na kudhoofisha suluhisho la mataifa mawili.
Mawaziri hao watajadili njia za kukabiliana na uamuzi wa serikali ya Israel wa kuanza taratibu za unyakuzi wa ardhi za Ukingo wa Magharibi kwa jina la “mali ya serikali,” kama sehemu ya mipango ya kulazimisha mamlaka ya utawala huo kwenye maeneo hayo.
Mnamo Februari 8, serikali ya Israel iliidhinisha maamuzi kadhaa yaliyolenga kufanya mabadiliko katika hali ya kisheria na kiraia katika Ukingo wa Magharibi, kwa lengo la kuimarisha udhibiti wake wa maeneo hayo.
Kwa upande wake, Ofisi ya Rais wa Palestina imeonya kuhusu “hatari ya uamuzi huo,” ikielezea uainishaji wa ardhi za Ukingo wa Magharibi kama “mali ya serikali” kuwa ni kielelezo cha “unyakuzi halisi” wa ardhi ya Palestina, ikisisitiza kwamba hatua hiyo ni “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na maazimio ya kimataifa.”
Tangu Israel ipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 8, 2023, jeshi la utawala huo limezidisha mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki, sambamba na kufanya mauaji, kukamatwa watu ovyo, kuwahamisha kwa mabavu na ujenzi wa vitongoji viipya vya walowezi wa Kizayuni, katika njia ambayo Wapalestina wanasema inalenga kutengeneza hali mpya katika maeneo hayo.