Iringa. Saa 11 alfajiri katika kituo cha mabasi Iringa, sauti ya Faraja Mfyagidzi husikika ikitangaza safari za Iringa–Makete–Njombe.
Akiwa amevalia sare ya ukondakta na tiketi mkononi, si rahisi kutambua kuwa msichana huyo mwenye miaka 26 ni mhitimu wa Shahada ya Ualimu kutoka Chuo Kikuu Katoliki cha Mbeya (CUCoM).
Faraja ni mzaliwa wa Makete mkoani Njombe, mama wa mtoto mmoja mwenye ndoto ya kusimama darasani kufundisha na kulea kizazi cha Taifa.
Alihitimu mwaka 2023 akiwa na matumaini ya kuajiriwa serikalini kama walimu wengine wengi. Hata hivyo, ajira haikupatikana kama alivyodhani.
Baada ya kuhitimu, alituma maombi na kusubiri kwa matumaini, kila simu ilipopigwa alidhani ni wito wa kazi, lakini kimya kiliendelea.
Wakati huohuo, majukumu ya maisha hayakusubiri kodi ya nyumba, chakula na mahitaji ya mtoto yalihitaji fedha kila siku.
Alijiuliza kama thamani yake ipo kwenye ajira ya Serikali pekee. Jibu alilolipata lilikuwa hapana. Aliamua kusimama na kupambana kwa kutumia fursa zilizopo.
Mwanzo wa kujitegemea
Hatua ya kwanza ilikuwa kuanzisha biashara ndogo ya mama lishe eneo la Mbalizi mkoani Mbeya. Kwa miezi sita alipika na kuuza chakula, akiamka alfajiri hulala usiku akiwa amechoka. Mapato hayakuwa makubwa, lakini yalikuwa halali na ya heshima.
Anasema hapo ndipo alipojifunza kuwa kazi haichagui mtu, ni mtu ndiye anayeipa kazi heshima. Kwa kuifanya kwa uadilifu, hata kuuza chakula ni kazi yenye thamani.
Baadaye alipata taarifa kupitia marafiki kuhusu nafasi ya ukondakta katika kampuni ya mabasi ya Japanese yanayofanya safari kati ya Iringa, Makete na Njombe. Bila kusita, aliamua kujaribu kuomba.
Kuvunja mipaka ya kijinsia
Sekta ya usafirishaji wa abiria kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume.
Siku ya kwanza kazini, Faraja anakiri kuwa alihisi woga. Alijiuliza kama ataweza na kama abiria watamkubali!
Anasema changamoto zilikuwepo. Wapo waliompuuza, wengine wakisema wazi kuwa kazi hiyo si ya wanawake. Maneno hayo yalimuumiza, lakini pia yalimuongezea nguvu ya kuthibitisha uwezo wake.
Aliamua kuweka mipaka ya heshima, kuzingatia nidhamu na kutumia lugha ya staha kwa abiria. Ndani ya muda mfupi, hali ilibadilika.
Abiria walianza kumzoea na kumheshimu kwa utendaji wake mzuri.
Neema Mlowe, mmoja wa abiria wa mara kwa mara, anasema Faraja ni kondakta anayefanya kazi kwa heshima na umakini.
Kauli kama hizo zimempa moyo na kumthibitishia kuwa uwezo haupimwi kwa jinsi.
Msimamo mbele ya jamii
Wazazi wake waliokuwa na wasiwasi mwanzoni walibadilika walipoona anavyopambana kwa heshima na kujitegemea.
Wenzake wa chuoni pia walishangazwa na uamuzi wake. Wapo waliomuuliza kwa nini hafanyi kazi ya taaluma yake na wengine wakihisi amejishushia hadhi.
Hata hivyo, Faraja anasema anaona fahari kujitafutia kipato halali. Anasema kuendelea kusubiri ajira rasmi bila kufanya kitu chochote si suluhisho, bali kufanya kazi yoyote halali ni bora kuliko kukata tamaa.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba hatua yake imekuwa chanzo cha hamasa kwa vijana wengine, hasa wanafunzi wa vyuo waliopo Iringa, wanaokiri kuwa wamejifunza kuwa hakuna kazi ndogo ilimradi ni halali na inafanywa kwa bidii.
Kujiendeleza kitaaluma
Faraja hakutosheka na uzoefu wa kazini pekee. Serikali ilipoanzisha utaratibu wa makondakta kuwa na mafunzo ya huduma kwa wateja, anasema alijiunga na masomo maalumu na Mei 2025 akapata cheti kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).
Kwa sasa Faraja ana leseni halali ya kufanya kazi hiyo kisheria. Hivyo, anasema mafunzo hayo yameongeza weledi wake na kuimarisha imani ya abiria pamoja na waajiri wake.
Maisha yanaendelea
Mapato anayopata yanamwezesha kulipa kodi, kuhudumia mahitaji ya mtoto wake na hata kuwasaidia wazazi wake kijijini.
“Furaha ya kununua mahitaji ya mtoto wangu kwa hela zangu mwenyewe ambazo ninazitafuta mwenyewe ni ushindi mkubwa,” anasema Faraja kwa furaha.
Licha ya kuwa kondakta, mwanadada huyo anasema ndoto yake ya kuwa mwalimu bado ipo. Hata hivyo, hajifungii kwenye wazo hilo pekee bali anasema anaamini maisha hayawezi kusimama yakisubiri barua ya ajira rasmi kutoka serikalini.
Anasisitiza kuwa, mwanamke anaweza kufanya kazi yoyote halali hata kama haijazoeleka kufanywa na wanawake au haimo kwenye taaluma aliyosomea.
Kwa mtazamo wake, Faraja anasema kuanza chini si kushindwa, bali ni hatua ya kuelekea juu.
Ujumbe kwa wanawake na vijana
Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, Faraja anawahimiza wanawake kuwa jasiri na kuchangamkia fursa halali.
Anasema wasichana wasione aibu kuanza na kazi ndogo, kwa sababu kila mafanikio makubwa huanzia kwenye hatua ndogo.
Leo hii, jina la Faraja Mfyagidzi linatambulika miongoni mwa abiria wa njia ya Iringa–Makete–Njombe si kama kondakta tu, bali kama mfano wa mwanamke aliyekataa kukata tamaa.
Safari yake inaonesha kuwa mafanikio si lazima yawe kwenye kile ulichokisomea pekee, bali kwenye namna unavyotumia kile kilicho mikononi mwako kwa wakati uliopo. Amechagua kufanya kazi kwa heshima, kujiendeleza na kuishi ndoto zake hatua kwa hatua.
Kwa Faraja, anasema hadhi ya mtu haipimwi na cheo alicho nacho, bali na ujasiri wa kusimama na kupambana pale ndoto zinapochelewa kutimia.