Chanzo cha picha, US Navy / Reuters
-
- Author, Amir Azimi
- Nafasi, BBC Persian Service
-
Muda wa kusoma: Dakika 6
Kuendelea kuongezeka kwa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati sasa hakuonekani tena kama onyo tu, bali kama maandalizi halisi ya hatua za kijeshi.
Kuwasili kwa kundi la mashambulizi la manowari ya kivita USS Abraham Lincoln karibu na Iran tayari ni tukio kubwa.
Manowari nyingine ya kivita, USS Gerald R. Ford, ilionekana hivi karibuni karibu na Mlango wa Gibraltar na inaelekea mashariki kusaidia operesheni. Marekani pia imependekeza chaguzi kadhaa za kijeshi na imeelekeza vifaa vingine vya kijeshi katika eneo hilo.
Chanzo cha picha, Reuters
Hatua hizi zinaweza kuwa njia ya kuimarisha diplomasia. Lakini pia zinaweza kuashiria kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yamekwama, na hatua za kijeshi zinaweza kufuata iwapo hakuna upande utakaobadilisha msimamo wake.
Hali hii inaleta swali muhimu: Kwa nini viongozi wa Iran, angalau hadharani, wanaonekana kupinga jeshi lenye nguvu zaidi duniani pamoja na mshirika wake mkuu katika Mashariki ya Kati?
Jibu linapatikana katika masharti ambayo Washington imeweka kwa ajili ya mazungumzo.
Chanzo cha picha, US Navy / Reuters
Masharti ya Marekani yanavyoonekana kama “kusalimu amri”
Kwa mtazamo wa Tehran, masharti haya si ya mazungumzo bali ni kusalimu amri.
Masharti hayo yanajumuisha, kusitisha urutubishaji wa madini ya urani, kupunguza umbali wa makombora ya masafa marefu ili yasitishie Israel, kusitisha kuunga mkono makundi yenye silaha katika eneo, na, kama alivyosema Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, kubadili namna Jamhuri ya Kiislamu inavyowahangaisha raia wake
Kwa viongozi wa Iran, haya si mambo madogo ya sera, bali ni nguzo kuu za usalama wa taifa.
Kwa miaka mingi, bila washirika wakubwa wa kimataifa, Iran imejenga kile inachokiita “Axis of Resistance”, mtandao wa makundi yenye silaha washirika wake, ulioundwa kuzuia migogoro kufika mipakani mwa Iran na kuongeza shinikizo dhidi ya Israel.
Chanzo cha picha, EPA
Mpango wa makombora ya masafa marefu wa Iran umechukua nafasi ya jeshi lake la anga lililozeeka, na umekuwa njia ya kujilinda kutokana na ukosefu wa teknolojia ya kisasa ya kijeshi.
Mpango wa nyuklia, ingawa unasemwa kuwa ni wa amani, unaonekana na wengi kama njia ya kujikinga dhidi ya vitisho.
Hata kama hautengenezi silaha za nyuklia, uwezo wa kurutubisha urani unaipa Iran uwezo wa msingi wa kutengeneza silaha hizo haraka endapo itaamua kufanya hivyo. Uwezo huu unaweza kutumika kama kadi ya shinikizo katika mazungumzo.
Kwa mtazamo wa Tehran, kuondoa mambo haya kutaharibu kabisa msingi wa usalama wake.
Chanzo cha picha, Iran Army Office / EPA
Hatari kwa kiongozi mkuu wa Iran
Kwa mtazamo wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kukubali masharti hayo kunaweza kuwa hatari zaidi kuliko vita vya muda mfupi na Marekani chini ya uongozi wa Trump. Vita, ingawa vina gharama kubwa, vinaweza kudhibitiwa bila kupoteza uwezo wote wa kimkakati.
Lakini hatari zilizomo katika hesabu hii ni kubwa, na sio kwa Irani tu.
Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Shambulio lolote la Marekani linaweza kuwalenga viongozi wakuu wa Iran mapema. Ikiwa Khamenei angeuawa, si tu kwamba utawala wake wa zaidi ya miaka 30 ungeisha, bali pia mpito wa uongozi ungeweza kuvurugika katika wakati nyeti.
Mashambulizi dhidi ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na vyombo vingine vya usalama vinaweza kudhoofisha mfumo wa serikali, hasa baada ya kurejesha udhibiti kufuatia ukandamizaji mkali wa maandamano ya hivi karibuni.
Wananchi wengi wameonyesha hasira kutokana na hali ngumu ya maisha.
Kushambuliwa kwa ghafla kwa serikali kunaweza kubadilisha usawa wa ndani kwa njia zisizotarajiwa
Chanzo cha picha, Reuters
Tehran inaweza kudhani kuwa Marekani itazingatia tu kudhoofisha mipango yake ya nyuklia na makombora. Kutokupiga hesabu vizuri kuhusu malengo, muda, au matokeo ya kisiasa kunaweza kupanua mzozo haraka.
Shinikizo la kiuchumi linafanya hali kuwa hatari zaidi. Uchumi wa Iran, ambao tayari umeathiriwa na vikwazo, mfumuko wa bei, na kushuka kwa uwezo wa kununua, utapambana na mshtuko zaidi. Matatizo ya usafirishaji wa mafuta nje au miundombinu iliyoharibiwa itaongeza hasira ya umma, ambayo imezuiwa lakini haijatatuliwa.
Katika hali hii, maandamano hayo yana malengo kadhaa na yanaonyesha azma kwa ulimwengu wa nje na nguvu kwa watu wa ndani ya Iran, lakini yanafanya mapatano kuwa magumu zaidi.
Chanzo cha picha, Reuters
Hatari kwa Washington
Hatari si kwa Iran pekee, bali pia kwa Washington.
Kwenye karatasi, jeshi la Marekani linaweza kufanikisha malengo ya rais wake ikiwa mvutano utaongezeka. Lakini vita havipiganwi kwenye karatasi. Mara nyingi huathiriwa na makosa ya maamuzi, kuongezeka kwa mapigano bila kukusudia, na matokeo yasiyotegemewa.
Chanzo cha picha, EPA
Migogoro ya hivi karibuni, ikiwemo mapambano ya siku 12 na Israel, imeonyesha udhaifu katika mifumo ya kijeshi ya Iran, lakini pia imeipa uzoefu wa namna ya kujifunza na kujirekebisha.
Vita vikubwa zaidi vinaweza kuleta matokeo yasiyotarajiwa kwa pande zote. Serikali dhaifu Tehran haimaanishi moja kwa moja utulivu au manufaa kwa nchi za Magharibi. Badala yake, pengo la madaraka linaweza kuibua makundi mapya yenye misimamo mikali na kufanya eneo hilo kuwa hatari zaidi.
Chanzo cha picha, Iran’s Supreme Leader Office via EPA
Ayatollah Khamenei ana chaguo chache.
Kukubali masharti ya Washington kunaweza kudhoofisha mkakati wa ulinzi wa Iran. Kuyakataa kunaongeza hatari ya mgogoro wa ndani katika taifa ambalo tayari ni dhaifu kiuchumi na kisiasa.
Kati ya kile wanachokiona kama “chaguo baya zaidi” ni kusalimu amri kimkakati, na “bora kati ya mabaya,” Tehran inaonekana, angalau hadharani, kuegemea upande wa pili.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid