Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amebeza madai yanayotolewa na maadui ya kutoshindwa na kusema kuwa maadui hawakutarajia kuiona nchi hii ikionyesha umadhubuti wake mbele ya kuendelea kukusanya majeshi katika kanda hii.

“Maadui wanadai kuwa hawawezi kushindwa, lakini hili ni dai la uongo,” amesema Meja Jenerali Amir Hatami katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Uongozi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC ) hii leo katika mji wa Tehran.

Amesema, adui hakutarajia kukabiliwa na irada mathubuti ya nchi hii licha ya kutuma meli za kubeba ndege na silaha nyingine. 

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ametamka haya kufuatia hatua ya Marekani ya kutuma meli za kubeba ndege za kivita na mifumo ya ulinzi katika eneo la Magharibi mwa Asia ikiwa ni pamoja na karibu na mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Meja Jenerali Hatami amesema: Msimamo wa karibuni wa kuchochea vita wa Marekani ulikuwa na lengo la kujaribu kuidhoofisha Iran hatua kwa hatua na kuwachosha watu wake na “adui anaamini kuwa tumedhoofika na yeye ndiye anayeshikilia mpini. Lakini ni mtazamo huu si sahihi, Iran kuu haiwezi kumezwa,” amesisitiza Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran na kusema: Leo hii, mamilioni ya wanajeshi nchini Iran wako tayari kujitolea maisha yao kwa ajili ya nchi yao.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameashiria uvamizi wa kijeshi wa Israel na Marekani mwezi Juni mwaka jana na jibu kali lililotolewa na nchi hii kwa hujuma hiyo na kusema: Katika kukabiliana na uchokozi huo, jeshi la IRGC lilishambulia shabaha nyeti na za kimkakati katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu kwa kustafidi na aina mbalimbali za makombora ya balistiki na hypersonic. 

Jeshi la IRGC pia lilishambulia kambi muhimu ya jjeshi la Marekani katika Asia Magharibi ya al Udeid huko Doha, Qatar kwa makombora kadhaa balistiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *