Mbozi. Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari amewataka washiriki wa mafunzo ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Shiwinga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kufanya kazi kwa uadilifu, uzalendo na weledi.
Jaji Asina ametoa wito huo Februari 23, 2026 baada ya kuwatembelea washiriki wa mafunzo hayo, yanayoendelea katika ukumbi wa Veronica katika mji wa Mlowo wilayani, yaliyoanza Februari 22, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa leo Februari 24, 2026.
Wasimamizi wa uchaguzi wa udiwani wakiwa wanapewa mafunzo Kwa ajili ya uchaguzi wa diwani kata ya Shiwinga wilayani Mbozi Mkoani Songwe
Akizungumza na washiriki, jaji huyo amewataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya kisheria ili kufanikisha uchaguzi huo mdogo kwa misingi ya haki na uwazi.
Amesisitiza umuhimu wa kufika vituoni mapema, kufanya maandalizi stahiki na kuhakikisha mchakato wa upigaji kura unazingatia muda na taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake, Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Zefania Msuva amesema mafunzo hayo ya siku tatu yanashirikisha washiriki 76 na yamelenga kuwajengea uwezo watendaji hao ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na amani.
Wasimamizi wa uchaguzi wa udiwani wakiwa wanapewa mafunzo Kwa ajili ya uchaguzi wa diwani kata ya Shiwinga wilayani Mbozi Mkoani Songwe
Amebainisha kuwa vyama vinane vitashiriki katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Februari 26, 2026. Wagombea ni Menati Mzumbwe (CCM), Matias Dulle (ADC), Elly Shitindi (Ada-Tadea), Mary Daud (UPDP), Neema Abadallah (UMD), Emily Siwale (SAU), Mussa Dulle (Makini) na Cosam Mwakyusa (TLP).
Uchaguzi mdogo wa Kata ya Shiwinga unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Lusako Mwalukomo (CCM.