Dodoma. Kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa mafua makali, homa na kikohozi, wakazi wa Jiji la Dodoma wametakiwa kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na maambukizi ambayo yanaenea kwa kasi.

‎Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dk Sebastian Pima, idadi ya wagonjwa wa mafua wanaofika vituo vya afya kutibiwa imeongezeka ambapo vipimo vinaendelea kuchukuliwa kuona kama ni ya kawaida au ni mlipuko.

‎Akizungumza na Mwananchi leo Februari 24, 2026, Dk Pima amesema ugonjwa uliopo ni mafua ya msimu ambayo huwa yanazuka kutokana na hali ya hewa, lakini baadaye yanaisha baada ya watu kupata matibabu.

‎Amesema kinachoendelea ni mafua ya msimu na kama inavyoeleweka virusi vya mafua huwa vinaenezwa kwa njia ya hewa na kushikana mikono, hivyo amewataka wananchi kujiwekea utaratibu wa kunawa mikono mara kwa mara ili kujiepusha na maambukizi.

“Haya ni mafua ya msimu yanatokana na hali ya hewa tuliyonayo ya mvua, ndiyo maana unaona watu wengi wanaumwa homa na kikohozi kinachosababishwa na mafua hayo,” amesema Dk Pima.

‎‎Amesema maambukizi ya mafua hayo yanaenea kwa kasi kutokana na watu kukaa kwenye msongamano hasa shuleni na maeneo ya kazi ambapo kama kuna mtu mmoja mwenye maambukizi anawaambukiza na wengine.

“Hii inatokana na kwamba huwa tunatoa mafua kwa kutumia mikono, sasa hiyo mikono isiposafishwa maambukizi yataenea kwa watu wengi bila kujua pale wanaposalimiana kwa kushikana mikono,” amesema.

Mganga mkuu wa Jiji la Dodoma, Dk Sebastian Pima.

‎Dk Pima amesema matibabu ya mafua hayo ni dawa za kawaida za kikohozi, dawa za homa na za mzio (allergies) ambazo wagonjwa huwa wanapatiwa wakifika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu kwani ugonjwa huo siyo wa kulazwa.

Wananchi wazungumza

‎Baadhi ya watu waliougua ugonjwa huo wametaja dalili ni mafua, kikohozi, homa na baadhi ya viungo vya miwili kama mikono na miguu kuuma.

‎Mkazi wa Swaswa, Salome Stephano amesema aliyeanza kuumwa ugonjwa huo alikuwa ni mtoto wake wa kidato cha pili, akafuatia mwanaye wa darasa la tano na mwisho wa siku na yeye akaupata.

‎Amesema mafua ni makali yanayosababisha homa na kichwa kuuma kupita kiasi, ambapo walipokwenda hospitalini kupata matibabu walipewa dawa za mafua ambazo zimewasaidia kwa kiasi kikubwa.

“Mimi nilipopata mafua hali yangu ilikuwa mbaya kwani nilipopelekwa hospitalini niliwekwa mapumziko na kutundikiwa dripu za maji tatu ndipo nilipata nafuu, kwa kweli hali ilikuwa mbaya nilikuwa siwezi kupumua vizuri,” amesema Salome.

‎Kwa upande wake, mkazi wa Nzuguni, Dotto Baliheza amesema homa hiyo imeingia kwenye familia yake ambapo yeye, mke wake na watoto wao waliumwa kwa kupokezana na hali haikuwa nzuri.

‎”Tumepona baada ya kwenda hospitalini kupata matibabu maana homa, mafua na kikohozi vilikuwa vimetuvamia lakini kwa sasa tunaendelea vizuri baada ya kupata dawa,” amesema Baliheza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *