Shinyanga. Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM), Patrobasi Katambi amemtaka mkandarasi wa miradi ya barabara ya Mwawaza na stendi ya mabasi, kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi kulingana na mkataba unavyosema.
Katambi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, amebainisha hayo Februari 23, 2026 baada ya ukaguzi wa barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza) na stendi ya mabasi ya mkoa iliyopo Kata ya Kizumbi huku akifurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Shinyanga.
“Hali inayoonekana hapa hairidhishi kabisa, nilitegemea utekelezaji uwe umefikia thamani ya pesa mliyotanguliziwa ya Sh3.9 bilioni, mkandarasi unatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha kazi kwa muda uliowekwa katika mkataba, hakuna muda utakaoongezwa, tuko radhi kuvunja mkataba kama mambo hayaeleweki,” amesema Katambi.
Kwa upande wake, mkandarasi wa miradi ya barabara na stendi, Edwin Rwezahura ameahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kamaliza kazi ndani ya muda kama ulivyopangwa kwenye mkataba wake.
Mwonekano wa hali ilivyo katika ujenzi wa stendi ya mabasi ya Mkoa wa Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda
“Tuko tayari kufanya kazi usiku na mchana katika miradi yote miwili ili kumaliza ndani ya muda ulioandikwa katika mkataba,” amesema Rwezahura.
Mhandisi wa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga ulioko kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, Ruburi Kahatano, ameeleza kuwa kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 95.
“Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Shinyanga umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki ni ukamilishaji wa jengo la abiria na majaribio ya vifaa kwa kutua ndege nyakati za usiku,” amesema Kahatano.
Historia ya mgogoro
Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mwawaza na stendi ya mabasi ulisainiwa Julai 2025 na Katambi, ukishuhudiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Shinyanga.
Januari 9, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita alikagua mradi wa barabara na kutoridhishwa na maendeleo, alitoa maagizo kwa mkandarasi kuongeza kasi ili kuendana na muda wa mkataba, baada ya siku hiyo mkandarasi aliondoa vifaa eneo la mradi.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Patrobas Katambi akifanya ukaguzi wa uwanja wa ndege uliopo kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda
Januari 29, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga alienda tena kukagua utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa katika mradi wa barabara na kukuta kama walivyoacha, ndipo alipochukua hatua ya kumwagiza OCD kuwaweka ndani mkandarasi na mkandarasi mshauri kwa kutotekeleza maagizo.
Ujenzi uwanja wa ndege
Mradi huo, mkataba wake ulisainiwa 2017 na kuanza kutekelezwa mwaka 2023 na kampuni ya Chico, ukigharimu Sh52 bilioni hadi kukamilika kwake na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege aina ya Bomberdier Q400.
Mwonekano wa Runway na jengo la abiria katika uwanja wa ndege uliopo kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.
Urefu wa uwanja ni kilomita 2.2 na upana ni mita 30, kikiwa ni feeder airport kwa viwanja vikubwa kama Mwanza na Dar es Salaam.