Msemaji wa serikali ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu inafadhilisha diplomasia kuliko vita, lakini inaviona viwili hivyo kama mikakati ya kulinda maslahi ya taifa la Iran.

Fatemeh Mohajerani amesema, “Ingawaje stratejia ya vikosi vyetu vya kijeshi inabaki kwenye ajenda, na maandalizi muhimu juu ya hayo yangalipo, kama ilivyoonekana kwenye mazoezi ya kijeshi ya karibuni, lakini njia ya diplomasia pia inafuatiliwa kwa nguvu. Tunafuatilia matukio yanayojiri kwa karibu, na tunaendelea kujitolea kwenye mchakato wa diplomasia.”

Amekumbusha kuwa, Iran ilikuwa katika raundi yake ya 6 ya mazungumzo na Washington mnamo Juni mwaka jana 2025 wakati Marekani ilipoungana na utawala wa Kizayuni wa Israel kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu.

Vita hivyo dhidi ya Iran vilichukua siku 12, huku muungano wa Israel na Marekani ukishindwa kutungua makombora ya Iran yaliyotua Tel Aviv na kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani Al-Udeid huko Qatar.

Maafisa wa Iran wanasisitiza kwamba, raundi mpya ya mazungumzo ya nyuklia lazima ihakikishe vikwazo vya haramu dhidi ya taifa hili vinaondolewa. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghch alifanya duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na Marekani huko Geneva, Uswisi kwa upatanishi wa Omana; mazumgumzo yasiyo ya moja kwa moja ambayo yumkini yakaendelea Alkhamisi.

Huku Marekani ikizidisha mvutano katika eneo la Asia Magharibi ili kutishia Iran kwa kupeleka manowari za kijeshi karibu na Ghuba ya Uajemi, Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kwamba, haitakubali kulazimishwa kusitisha kikamilifu urutubishaji wa urani na kueleza kwamba, makombora ya Iran hayana nafasi katika mazungumzo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *