Karibu risasi elfu moja zilifyatuliwa na wanajeshi wa Israel katika mauaji ya kiholela dhidi ya wafanyakazi wa misaada huko Tel al-Sultan, Gaza, huku baadhi yao wakiuawa kwa kupigwa risasi kwa karibu, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hivi karibuni.

Mashirika huru ya utafiti ya Earshot na Forensic Architecture yametoa ripoti ya kina kwa kutegemea simulizi za mashahidi na uchambuzi wa sauti na taswira, yakithibitisha kuwa wafanyakazi kadhaa wa misaada waliuawa katika mashambulizi hayo, ambapo angalau mmoja wao alipigwa risasi kutoka karibu, umbali wa mita moja tu.

Mashirika hayo yameelezea mauaji hayo ya Machi 23, 2025, huko Tel al-Sultan, magharibi mwa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza kama “mojawapo ya nyakati mbaya zaidi” za vita kwa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina (PRCS). 

Wafanyakazi 15 wa kutoa misaada waliuawa katika shambulio hilo, wakiwemo wahudumu wa afya kutoka Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina (PRCS), wazimamoto kutoka Idara ya Ulinzi wa Raia wa Palestina (PCD) na mfanyakazi mmoja wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).

Wafanyakazi hao wa kutoa misaada waliouawa katika jinai hiyo ya kuogofya ya Wazayuni, walizikwa pamoja na magari yao. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, walipowafikia wafanyakazi wa misaada, wanajeshi wa Israel waliingia katikati yao na magari yao na kuwaua baadhi yao kwa kwa kuwapiga risasi kwa karibu.

Mashirika huru ya utafiti ya Earshot na Forensic Architecture yamesema katika ripoti hiyo kwamba, wanajeshi wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji hayo kwa makusudi na kisha kuficha na kuvuruga ushahidi wa shambulio hilo kwa njia mbalimbali.

Vikosi vya Israel vimeshutumiwa mara kwa mara kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika vita vyao vya mauaji ya halaiki huko Gaza, ambavyo mpaka sasa vimewaua shahidi zaidi ya Wapalestina 72,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *