Msemaji wa waasi wa M23 ameripotiwa kuuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za habari zimeripoti kuwa, Msemaji wa waasi la M23, Willy Ngoma, aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za jeshi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumanne.

Shirika la habari la Reuters limenukuu mwanadiplomasia wa kikanda, afisa mwandamizi wa M23 na mshauri wa serikali wa DRC wakithibitisha habari za kuuawa Ngoma. Hata hivyo hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu mauaji ya Msemaji huyo wa M23.

Haya yanaripotiwa siku moja baada yau wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Kongo DR kudai kuwa wamewauwa wapiganaji 50 waliokuwa wanachama wa kundi la waasi wa M23 na kuwateka nyara kadhaa katika mapigano makali ya hivi karibuni.

Kundi hilo lenye mfungamano na serikali ya Kinshasa kwa jina la Wazalendo limesema kuwa mapigano hayo yalijiri tarehe 16 na 22 mwezi huu wa Februari.  Limesema kuwa, wapiganaji wake waliyateka maeneo kadhaa huko Masisi, Rutshuru na Walikale katika jimbo la Kivu Kusini na pia Fizi huko Kivu Kaskazini kufuatia mapigano kati yao na muungano wa waasi wa M23. 

Kabla ya hapo, Lawrence Kanyuka, Msemaji wa waasi wa M23 aliituhumu Kinshasa kuwa imekiuka usitishaji vita mara kadhaa na kufanya hujuma za mara kwa mara na za kiholela katika maeneo yenye wakazi wengi huko Rumbishi.

Kadhalika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) iliripoti hivi karibuni kuwa, raia 50 waliuawa wakati wa mapigano yaliyozuka mwezi uliopita Januari kati ya vikosi vinavyoiunga mkono serikali na waasi wenye silaha wenye mfugamano na M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *