Rais wa mpito wa Madagascar, Michael Randrianirina amesema kwamba, nchi hiyo inatazama ushirikiano na jumuya ya BRICS kama njia ya kuelekea kwenye fursa mpya za kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Russia Today wakati wa ziara yake mjini Moscow, Randrianirina amesisitiza kwamba, nchi yake imeazimia kupanua machaguo yake ya kidiplomasia na kiuchumi.

“Ushirikiano na BRICS utafungua milango mipya,” Rais wa mpito wa Madagascar amesema na kuongeza kuwa, Madagascar inataka “kufanya kazi na nchi zote.”

Wiki iliyopita, Randrianirina alifanya mazungumzo na Rais wa Russia, Vladimir Putin na kuelezea utayarifu wa Antananarivo wa kufungua ukurasa mpya wa uhusiano na Moscow.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova alisema hivi karibuni kuwa, Moscow iko tayari kuimarisha ushirikiano na nchi wanachama na zinazotaka kujiunga na kundi la kiuchumi la BRICS ili kukabiliana na mashinikizo ya vikwazo haramu vya Marekani.

Viongozi wa nchi za BRICS wamekuwa wakililielezea kundi hilo kama jukwaa muhimu la kuimarisha maingiliano na uhusiano wa kiuchumi na kisiasa miongoni mwa nchi wanachama.

Kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin wa Russia, kundi la BRICS limelishinda kundi la G7 linalotawaliwa na nchi za Magharibi, kwa Pato Ghafi la Taifa (GDP). Putin alisema “Nchi wanachama wa BRICS sio tu wanachangia theluthi moja ya ardhi ya dunia, na karibu nusu ya idadi ya watu wa sayari hii, lakini pia zinachangia asilimia 40 ya uchumi wa dunia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *