Leo ni Jumatabo Ramadhani 7 mwaka 1447 Hijria sawa na 25 Februari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita yaani tarehe 7 Ramadhani mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume (saw) katika mji wa Makka.

Baada ya kufariki dunia Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad (saw), Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume, na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikuraishi.

Baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina waliziidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihama kutoka Makka kwenda Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.  ****

Katika siku kama ya leo miaka 1246 iliyopita Ma’mun, khalifa wa utawala wa Bani Abbas alimlazimisha Imam Ridha (as) kukubali takwa lake la kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake.

Ni vyema kuashiria kuwa uadui wa watawala wa kizazi cha Bani Umayyah na Bani Abbas dhidi ya Ahlul-Baiti wa Mutume (saw) ni wa muda mrefu. Vizazi hivyo viwili ni maarufu kwa dhulma, ukandamizaji na utesaji dhidi ya Ahlul-Bayti wa Mtume, ambapo havikusita hata kuwaua maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume wa Allah. Baada ya Ma’mun kutwaa madaraka ya ukhalifa alihofia sana taathira chanya ya Imam Ridha (as) kwa watu na kwa kuwa alikusudia kumuweka mtukufu huyo chini ya uangalizi wake mkali, huku akijionyesha kuwa mwenye mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume, hivyo alitoa amri ya kumuondoa Imam Ridha kutoka Madina na kumpeleka Khorasan (Mash’had ya leo) na kisha akamlazimisha kukubali kuwa mrithi wa kiti cha ufalme.

Siku kama ya leo, yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka 201 Hijiria, khalifa huyo aliwasilisha mbele ya mtukufu huyo suala hilo ambapo hata hivyo alilipinga. Baada ya kulipinga, mtawala huyo dhalimu alitumia vitisho dhidi ya Imam Ridha (as) ambapo baadaye alikubali tu kwa kutikisa kichwa huku mtukufu huyo akisisitiza kuwa jambo hilo halitofikiwa.

Baada ya hapo mtukufu huyo alitumia fursa hiyo kuweza kueneza mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu suala ambalo baadaye lilimfanya Ma’mun kuchukizwa na hatua yake ya kumtoa mjini Madina na ni baada ya hapo ndipo akapanga njama ya kumuua, njama ambayo ilitekelezwa sawa na tarehe 30 Swafar mwaka 203 Hijiria.  ***

Katika siku kama hii ya leo miaka 42 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad.

Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.    *****

Tarehe 25 Februari miaka 40 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake.

Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo.

Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.    ****

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita Mzayuni aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada kwa jina la Baruch Goldstein aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao.

Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani.

Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani! ***

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *