Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema Iran na Marekani zina “fursa ya kihistoria” iliyopo mbele ya macho ya kufikia “makubaliano ambayo hayajawahi kushuhudiwa,” huku akionya kwamba Jamhuri ya Kiislamu italinda uhuru na mamlaka yake ya kujitawala kwa gharama yoyote endapo kutakuwa na uvamizi mpya wa kijeshi wa Marekani.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha hayo katika mfululizo wa jumbe alizoweka kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumanne, akitoa maoni yake kuhusu duru ya tatu inayosubiriwa ya mazungumzo mapya ya nyuklia kati ya pande hizo mbili ambayo yanatarajiwa kufanyika mjini Geneva kesho Alkhamisi Februari 26.

Makubaliano kama hayo, amesema Araghchi, yanaweza kushughulikia “wasiwasi wa pande zote mbili” na kufanikishwa “maslahi ya pande zote mbili.”

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametanabahishwa kuwa, uwezekano wa kufikiwa mwafaka unategemea diplomasia “kupewa kipaumbele,” na akashauri kwamba Marekani isiathiri mchakato mpya wa kidiplomasia kwa kuanzisha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kama ilivyokuwa wakati wa mazungumzo ya awali kati ya nchi hizo Juni iliyopita.

Kwa upande wa Jamhuri ya Kiislamu, ametoa hakikisho kwamba imeazimia “kufikia makubaliano ya haki na usawa – katika muda mfupi kabisa uwezekanao.”

Wakati huo huo, Araghchi amesisitiza tena kuhusu kanuni za msingi za Jamhuri ya Kiislamu kuhusu mpango wake wa nishati ya nyuklia wenye malengo ya amani.

“Misimamo na imani zetu za msingi ziko wazi kabisa: Iran haitatengeneza silaha ya nyuklia katika hali yoyote ile; lakini wakati huohuo, sisi Wairani hatutaacha haki yetu ya kutumia manufaa ya teknolojia ya nyuklia ya malengo ya amani kwa ajili ya watu wetu”, amesisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Wakati huo huo, Araghchi amesisitiza kuwa muelekeo wa Iran kuhusiana na mazungumzo hautaathiri mamlaka ya kujitawala ya taifa.

“Tumethibitisha kwamba hatutasita kufanya chochote kulinda mamlaka yetu ya kujitawala kwa ujasiri. Ujasiri huo huo, tunakwanda nao kwenye meza ya mazungumzo, ambapo tutafuatilia kupatikana suluhisho la amani juu ya tofauti zozote (zilizopo)”, amebainisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Hayo yanabainishwa huku Marekani ikiwa imeshamirisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na kandokado ya Iran, kwa kutuma manowari mbili za kubebea ndege za kivita pamoja na ndege nyingi za kivita na mitambo ya makombora.

Matamshi ya Araghchi yametilia mkazo tena msimamo ambao umeshabainishwa hapo kabla na viongozi wengine waandamizi wa Iran, wa kuionya Washington na washirika wake wa kutoitumia fursa ya Tehran kushiriki katika mchakato wa kidiplomasia kuanzisha uchokozi mpya wa kijeshi usio na ulazima wala uhalali wa kisheria…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *