
Kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema, Rais wa Marekani Donald Trump anasema uwongo kuhusu Iran.
Hakeem Jeffries ameyasema hayo kufuatia mkutano wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Robio na wawakilishi wakuu wa Bunge wa kuizungumzia Iran.
“Mwaka jana, tuliambiwa kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa umeangamizwa kikamilifu,” ameeleza Jeffries mbele ya waandishi wa habari na kuongezea kwa kusema: “sasa tunatakiwa kuamini kwamba kuna hali ya dharura ambayo inaweza kumfanya Donald Trump ahitaji kuchukua hatua za kijeshi tena ili kuizuia Iran isifikie malengo yake ya nyuklia. Ilikuwaje basi kuhusu yale madai ya kuuangamiza kikamilifu na moja kwa moja mpango wa nyuklia wa Iran?”
Jeffries amefafanua kwa kusema: “Ni wazi kwamba, ama yeye (Trump) aliwaambia uwongo Wamarekani, au anasema uwongo hivi sasa. Kwa hiyo katika kipindi hiki, chochote atakachosema hakitakuwa na maana kwa Wamarekani”.
Kiongozi huyo wa Wademocrat katika Bunge la Marekani amesisitiza: “Nitapenda kusikiliza kile ambacho maafisa wa serikali yake watasema katika kikao hiki cha faragha. Lakini pia ninakusudia kuwashinikiza kuhusu madai ambayo Donald Trump mwenyewe ametoa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kwamba kuna uharaka gani mkubwa sasa hivi mpaka mumekusanya manowari kubwa na kutaka kuitumbukiza Marekani kwenye vita vingine vya nje, vya muda mrefu na vya kufeli; vita ambavyo ni hakika kuwa vitasababisha madhara kwa Wamarekani…/