
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na mwenzake wa Gambia wamesisitiza haja ya kusimamisha uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili katika nyanja zote zenye maslahi ya pande mbili.
Katika mazungumzo ya simu Jumanne usiku, Sayyid Araghchi amemnyooshea mkono wa pongezi Mamadou Tangara, Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia, serikali, na watu wa nchi hiyo ya Kiafrika kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Araghchi ameelezea utayarifu wa Iran wa kuendeleza uhusiano wa pande mbili pamoja na kuratibu misimamo inayolandana katika ngazi ya mashirika ya kimataifa.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia, Mamadou Tangara amempongeza Araghchi, serikali, na watu wa Iran kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Amesisitiza azma ya serikali yake ya kupanua uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizi mbili. Pande hizo mbili zimetathmini njia za kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, pamoja na kujadili matukio ya kikanda na kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, Julai mwaka 2024, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Gambia zilirejesha uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kusimama kwa takriban miaka 14.
Iran na Gambia zimekubaliana kustawisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali; zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, uwekezaji, biashara na utamaduni, ambazo zinaweza kuhudumia maslahi ya mataifa yote mawili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Gambia.
Rais Masoud Pezeshkian alisema karibuni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kwa dhati kupanua ushirikiano wa kina na nchi za Afrika, kwa mujibu wa sera yake ya “diplomasia yenye mlingano” na msisitizo wa maslahi ya pamoja.