Nianze kwa kumpongeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kamishna Jenerali Areta Lymo, kwa kazi kubwa ambayo amefanya. Naendelea kufuatilia mahojiano yake na waandishi wa habari wa Mwananchi, na nimekoshwa kwenye eneo la kupunguza mateja Dar es Salaam. Hii ni kweli.

Watu hawaoni matokeo chanya na kuyageuza mjadala. Hasi hujadiliwa zaidi. Watumiaji wa dawa za kulevya walikuwa ghasia kubwa, katika vituo vya daladala mpaka makutano ya barabara. Watu kuporwa mali zao, na kujeruhiwa, ilikuwa kawaida.

DCEA kujitokeza na kueleza walivyofanikisha kukabili tatizo hilo, kwanza kwa kufanya dawa za kulevya kuwa adimu mitaani, pili kuwachukua mateja na kuwaweka kwenye kliniki za kuwasaidia kuondokana na uraibu, ni jambo jema. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Mateja bado wapo. Dawa za kulevya zipo.  Watu wanaendelea kutajirika kwa kuua nguvu kazi ya taifa letu.

Nimesoma sehemu ya mahojiano hayo Kamishna Lyimo akisema wanapokea vitisho, vilevile akibainisha kwamba kazi kubwa mbele yao ni kuwapata wauza unga, ambao amewaita wafadhili. Ni wale ambao hawaungwi na mnyororo unaotoka kwa mtumiaji wa mwisho, ila ndiyo wenye mali.

Lyimo anajua, si vibaya kumkumbusha kuwa kanuni ya kuu ya vita dhidi ya dawa za kulevya ni “Trust No One”, yaani usimwamini mtu. Vita dhidi ya dawa za kulevya inataka anayechunguza naye achunguzwe. Watu wenye kuendesha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hutakiwa kuchunguzwa kama wanafanya kazi sawasawa kwa ukweli na uaminifu.

Ni kama ambavyo wauza unga wanavyochunguzana wao kwa wao. Siku hata siku hufuatiliana kuona nani hufanya mawasiliano na polisi au kuwa karibu na mamlaka za Serikali. Sababu ni uwepo wa mapandikizi (snitches). Serikali kupitia mamlaka za kupambana na dawa za kulevya, hupenyeza wapelelezi wao ndani ya mitandao ya wauza unga ili kupata taarifa zote kamili na kuzifanyia kazi.

Wauza unga pia hupenyeza watu wao serikalini hususan kwenye mamlaka za udhibiti wa dawa za kulevya, hivyo kuwa wanapata kila kitu kutoka serikalini. Taarifa hizo huzitumia kuizidi ujanja Serikali na kuendelea kufanya biashara hiyo haramu kwa kujiachia.

Siri moja kubwa ya wauza unga kufanikiwa duniani kote ni kuwashika baadhi ya watu muhimu kwenye mamlaka za nchi. Hilo linawezekana kwa sababu kwenye dawa za kulevya kuna fedha nyingi mno.

Unakuta genge moja la wauza dawa za kulevya lina fedha zenye kutosha kuendesha Serikali moja ya Ulaya, acha Afrika. Watu hao wanashindwa vipi kuwa mabosi wa viongozi serikalini? Ndiyo maana mfumo ni kuchunguzana.

Sasa basi, kama kweli Kamishna Lyimo anataka kuweka alama kuwa wakati wake alifanikiwa kudhibiti dawa za kulevya nchini ni lazima asimwamini mtu. Vita dhidi ya dawa za kulevya ni mapambano ya kikauzu. Hakuna kumchekea mtu wala kumchukulia poa yeyote.

Hakuna wa kumruka kuwa yeye ni msafi. Vita dhidi ya dawa za kulevya ni mapambano ya ndani na nje. Ndani serikalini wahusika lazima wachunguzane kisha nje kuyachunguza magenge ya wauza unga na mitandao yao.

Uchunguzi wa ndani ni muhimu zaidi kuliko ule wa nje. Maana wanaopiga vita dawa za kulevya hupaswa kuwa watu wasafi, wenye kufanana na mapambano yenyewe. Ukiwa na mapandikizi ya wauza unga ndani mifumo ya Serikali matokeo yake ni kushindwa vita na wauza dawa za kulevya.

Inatakiwa mwendo uwe wa kunusana. Yule ambaye ananuka harufu ya mihadarati anafanyiwa kazi zaidi. Kipindi akichunguzwa ili apewe haki yake kulingana na uhalifu wake, vilevile anawekwa mbali asiweze kujua siri za mapambano akawa anaiteta Serikali kwa wahalifu wenzake.

Huwezi kufanikiwa vita dhidi ya dawa za kulevya kama kutakuwa na hali ya kuamini watu bila kujiridhisha nao. Hata baada ya kujiridhisha inatakiwa kuwapitia kila baada ya muda kuona kama bado wapo kwenye mstari.

Wataalamu wa mabadiliko ya tabia za binadamu wanasema kuwa kila baada ya wiki mbili binadamu huweza kubadilika. Hivyo, mtu anaweza kuwa msafi leo lakini wiki mbili zijazo akaanza kuingiwa na mabadiliko ya kitabia.

Mamlaka ya kwanza iliyoundwa kuchunguza na kudhibiti dawa za kulevya Marekani, iliongozwa na Kamishna Harry Anslinger. Huyu mtu alikuwa mkali hasa wa makundi ya wauza dawa za kulevya.

Anslinger alikuwa anavamia maskani za wauza unga na aina zote za dawa za kulevya na kukamata wahusika, kuchoma moto mihadarati na kadhalika. Hata hivyo, ni wakati ambao dawa za kulevya zilishamiri sana.

Ni wakati ambao ilielezwa kuwa Anslinger alipata utajiri wa haraka. Kwamba Anslinger pamoja na ukali wake kwenye dawa za kulevya, upande wa pili yeye mwenyewe alikuwa mnufaika wa biashara hiyo. Kwa mantiki hiyo, wauza waunga wajanja walimshtukia Anslinger na kugundua bei yake. Hivyo wakawa wanamzunguka.

Ipo dhana kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa ukaguzi wa uadilifu kupitia mtindo wa maisha ya watu, yaani lifestyle audit, kwamba kipindi cha wiki mbili ni kikubwa mno kutosha kumfanya binadamu awe wa tofauti. Kamishna Lyimo azingatie hili ndani ya ofisi yake. Je, watu anaofanya nao kazi wapo safi siku zote?

Ripoti za Ofisi ya Dawa na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa (UNODC) mwaka 2017, zilionesha kuwa thamani ya uhalifu wa mipango (organized crime) kwa jumla, kwa asilimia 50 unabebwa na dawa za kulevya.

Mantiki hapo ni kuwa dawa za kulevya ndiyo uhalifu wenye thamani kubwa zaidi duniani.

Ripoti hiyo ilionesha kuwa mzunguko wa kifedha wa biashara ya dawa za kulevya duniani kwa mwaka ni dola 652 bilioni ambazo kwa sarafu ya Tanzania ni Sh1,695 2 trilioni. Utaona kuwa fedha hizo ni nyingi mno zenye kutosha kuendesha bajeti ya nchi yoyote duniani.

Hayo ni makisikio. Mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni vita dhidi ya fedha nyingi. Lyimo ajue hilo. Yuda alimuuza Masihi, Yesu, sababu fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *