Wamiliki wa viwanda nchini wameshauriwa kutumia nembo ya Taifa ya ‘Made in Tanzania’ katika bidhaa na huduma wanapozalisha na kuzipeleka kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, ili kuongeza thamani na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 25, 2026 na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Lulu Mkudde, wakati wa mkutano wa wadau na wamiliki wa viwanda uliolenga kuhamasisha usajili wa nembo ya bidhaa na huduma ya ‘Made in Tanzania’ pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuitumia.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkude amesema kuwa ‘Made in Tanzania’ ni utambulisho rasmi wa huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini. Ameeleza kuwa nembo hiyo ilizinduliwa rasmi mwaka jana katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, maarufu Sabasaba na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Amefafanua kuwa ili mfanyabiashara aweze kusajili nembo hiyo, anatakiwa kuhakikisha kuwa bidhaa anazozalisha zinatumia walau asilimia 30 ya malighafi zinazopatikana nchini.

Amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa nembo hiyo, mwitikio wa wafanyabiashara umekuwa mkubwa, huku TanTrade ikifanya ziara katika kanda mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu usajili na matumizi ya nembo hiyo.

Mkudde ameeleza kuwa lengo kuu la usajili wa nembo ya ‘Made in Tanzania’ ni kuongeza thamani ya bidhaa, kusaidia ajenda ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda na kuzitambulisha bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Ni fahari yetu kutumia nembo ya Taifa. Tujivunie vya kwetu kwa kujenga uchumi wa nchi yetu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa TanTrade, Boniface Mrema, amesema kuwa nembo ya Taifa itawawezesha wazalishaji kupata masoko ya nje, hususan katika fursa zilizopo ndani ya Soko Huru la Afrika (AfCFTA), soko la African Growth and Opportunity Act (Agoa) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kwa muda mrefu kukosekana kwa nembo ya Taifa kulisababisha baadhi ya bidhaa za Tanzania kupoteza fursa za kimataifa, huku wengine wakizitumia zinazozalishwa nchini na kuziwekea nembo za mataifa yao, jambo lililoathiri mapato na utambulisho wa Tanzania kibiashara.

Mrema amewahimiza wadau kuboresha bidhaa zao ili kufikia viwango vinavyohitajika na kukidhi vigezo vya kutumia nembo ya ‘Made in Tanzania’, ili waweze kunufaika na masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Naye mwakilishi kutoka Kiwanda cha Uzalishaji Chumvi cha Bagamoyo Sea Salt, Damiano Semafali, amesema kuwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania zinapaswa kufahamika kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa kuna bidhaa nyingi kutoka nje zinazoingia nchini.

Amesema ni wajibu wa wazalishaji wa ndani kutumia nembo ya ‘Made in Tanzania’ kama sehemu ya mkakati wa kutangaza na kukuza bidhaa zinazozalishwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *