Tunduru. Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 1.7 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami ni kipande cha Boma–Mkwanda chenye urefu wa mita 700 na Mlingotini–Supermarket chenye urefu wa kilomita 1.

Akizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Tunduru kupitia ACT – Wazalendo, Ado Shaibu wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo leo Jumatano, Februari 25, 2026, Msimamizi wa mradi huo, Maura Juma amesema kuchelewa kwa ukamilishaji wa mradi kumesababishwa na mvua zilizoanza kunyesha mapema katika halmashauri hiyo.

Amesema pindi mvua zitakapopungua, ujenzi utaendelea kwa kasi na kuwaomba wananchi wanaotumia barabara hizo kuwa wavumilivu wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi huo.

“Niwaombe wananchi wawe na subira. Mradi huu umegharimu takribani Sh800 milioni na utamalizika mwaka huu ili kuwawezesha wananchi kutumia barabara hizo bila changamoto,” amesema Juma.

Katappira likiwa eneo la kazi kwa ajili ya kusambaza kifusi katika barabara ya Boma Mlingotini

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Tunduru, Petro Damiani amesema mradi huo wa barabara za lami unatarajiwa kugharimu Sh800 milioni.

Amefafanua kuwa mkandarasi alikabidhiwa mradi huo Julai 2025 na ilitarajiwa ukamilike Januari 2026, lakini mvua zilizoanza kunyesha tangu Oktoba mwaka jana, zimeathiri utekelezaji wake.

“Ndani ya miezi miwili ijayo mradi utakuwa umekamilika na wananchi wataendelea kutumia barabara zao kwa urahisi,” amesema Damiani.

Hata hivyo, Shaibu hakuridhishwa na maelezo ya wataalamu hao na kuwataka kuongeza kasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Pia, ameitaka Tarura kuhakikisha inazingatia hali ya jiografia ya maeneo husika kabla ya kuingia mikataba na makandarasi.

“Si sahihi mradi uliokabidhiwa Julai mwaka jana hadi sasa Februari haujakamilika, ilhali ulitakiwa kumalizika Januari. Naiomba Tarura mkaze buti ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila vikwazo,” amesema Shaibu.

Mmoja wa waendesha bodaboda wanaotumia barabara hizo, Hamisi Mohamed amesema kukamilika kwa barabara hizo kutarahisisha shughuli zao za kila siku.

Amesema kwa sasa wanalazimika kutumia njia mbadala zilizo mbali zaidi kwa hofu ya kuharibu pikipiki zao kutokana na hali mbaya ya barabara zinazoendelea kujengwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *