Paris, Ufaransa. Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, ameitwa mahakamani kujibu tuhuma za ubakaji zinazomkabili na huenda akakumbana na kifungo cha hadi miaka 15 jela endapo atapatikana na hatia.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Februari 2023, baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 wakati huo kudai kuwa alibakwa katika nyumba ya mchezaji huyo iliyopo Val-de-Marne, kusini mashariki mwa Paris.

Hakimi, ambaye ni raia wa Morocco, amekanusha vikali tuhuma hizo. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, akieleza kuwa yuko tayari kusimama mahakamani ili ukweli ujulikane.

Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, ambaye ni raia wa Morocco, ameeleza kuwa yuko tayari kusimama mahakamani ili ukweli ujulikane. Picha na Mtandao

“Leo, tuhuma ya ubakaji inatosha kupelekea kesi kusikilizwa. Hii si haki kwa wasio na hatia wala kwa waathirika wa kweli. Ninasubiri kwa utulivu kesi hii ili ukweli ujitokeze hadharani,” ameandika nahodha huyo wa Morocco.

Wakili wake, Fanny Colin, amethibitisha kuwa kesi hiyo imepelekwa mahakamani, huku akidai kuwa tuhuma zinategemea ushahidi wa upande mmoja pekee. Amesema mlalamikaji amekataa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, vipimo vya DNA na hata kuruhusu simu yake kuchunguzwa.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, mlalamikaji amedai kuwa amemfahamu Hakimi kupitia Instagram, Januari 2023, kabla ya kwenda nyumbani kwake kwa teksi iliyoandaliwa na mchezaji huyo. Ameeleza kuwa alibusu na kuguswa bila ridhaa yake kabla ya kudai kuwa alibakwa. Amesema aliweza kujinasua na kumtumia ujumbe rafiki yake aliyekwenda kumchukua.

Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji. Picha na Mtandao

Katika mfumo wa sheria wa Ufaransa, hatua ya kufunguliwa mashtaka ya awali humaanisha kuwa majaji wanaamini kuna viashiria vya kosa, lakini uchunguzi zaidi hufanyika kabla ya kesi kuanza rasmi.

Kocha wa PSG, Luis Enrique, alipoulizwa kuhusu sakata hilo kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya AS Monaco, amejibu kwa ufupi: “Hili liko mikononi mwa vyombo vya sheria.”

Hakimi, aliyezaliwa Hispania na kukulia katika akademi ya Real Madrid kabla ya kuchezea pia Borussia Dortmund na Inter Milan, alijiunga na PSG mwaka 2021.

Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, wakati alipokuwa na mke wake, Hiba Abouk, kabla ya wawili hao kuachana 2023. Picha na Mtandao

Wakati tuhuma hiyo ikiendelea, Hakimi aliwahi kukumbwa na tukio lingine, dhidi ya aliyekuwa mke wake, Hiba Abouk ambaye aliwasilisha kesi ya talaka Machi 27, 2023, akidai kugawiwa nusu ya mali ya mumewe.

Hata hivyo, baada ya tathmini ya mahakama, ilibainika kuwa Hakimi hakuwa na mali yoyote iliyosajiliwa kwa jina lake. Nyumba, magari na mali nyingine zote zilionekana kusajiliwa kwa jina la mama yake mzazi, Fatima.

Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, akiwa pamoja na mama yake mzazi, Fatima. Picha na Mtandao 

Ripoti zilieleza kuwa hata asilimia 80 ya mshahara wake wa kila mwezi unaokadiriwa kufikia Euro 1 milioni (zaidi ya Sh2.5 bilioni) huwekwa katika akaunti ya mama yake.

Taarifa za mahakama zilidai kuwa Hakimi hana mali, magari, nyumba wala vito vilivyosajiliwa kwa jina lake, na kwamba anapohitaji kitu hununuliwa na mama yake.

Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, wakati alipokuwa na mke wake, Hiba Abouk, kabla ya wawili hao kuachana 2023. Picha na Mtandao

Inadaiwa Abouk alitarajia kupata mgawo wa hadi Euro 70 milioni katika mchakato wa talaka, lakini alikumbana na mshangao baada ya kubaini kuwa nyaraka rasmi zinaonyesha mali zote si zake moja kwa moja.

Sasa mustakabali wa nyota huyo uko mikononi mwa mahakama, huku akisubiri kusikilizwa kwa kesi ambayo inaweza kuwa na athari kubwa katika maisha yake ya soka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *