
MSHAMBULIAJI wa Pyramids FC na timu ya taifa ya DR Congo, Fiston Mayele amemaliza ukame wa siku 122 baada ya juzi kufunga bao la Ligi Kuu ya Misri katika mechi ya ushindi wa mabao 3-1 wa timu hiyo dhidi ya Ghazl El Mahallah.
Mara ya mwisho kwa nyota huyo wa zamani wa Yanga kufunga katika Ligi hiyo ya Misri ilikuwa Oktoba 21 mwaka jana wakati wakiizamisha Pharco kwa mabao 2-0 na baada ya hapo Mayele hakufanikiwa kufunga tena hadi hiyo juzi.
Hilo linakuwa ni bao la tatu kwa Mayele kwa msimu huu kupitia mechi 16 kati ya 17 ilizocheza timu hiyo iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 37 ikitofautiana pointi moja na watetezi Al Ahly iliyopo nafasi ya tatu.
Nyota huyo ameweka rekodi ya kufikisha jumla ya mabao 50 na anakuwa mfungaji bora zaidi katika historia ya Pyramids FC tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Misri mwaka 2023, kabla ya hapo hakuna mchezaji aliyefikisha idadi hiyo.
Msimu wa kwanza katika mechi 32 mshambuliaji huyo wa zamani wa AS Vita ya Congo alifunga mabao 17, huku ule uliofuata alifunga 18 kupitia mechi 23 na msimu huu tayari kaweka matatu.
Katika mashindano ya kimataifa msimu uliopita Mayele alifanya vizuri akiibuka na kiatu cha ufungaji bora wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiweka kambani mabao sita na kuipa ubingwa chama hilo.
Mshambuliaji huyo amekuwa na muendelezo mzuri wa upachikaji mabao kwani kabla ya kutimkia Misri alipokuwa Yanga msimu wa 2022 alimaliza na mabao saba kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
Katika ligi ndani ya misimu miwili ya ligi alifunga mabao 35, msimu wa kwanza mabao 17 kupitiamechi 17 na ule uliofuata alionyakua kiatu cha mfungaji bora akiweka kambani mabao 18 kwa kucheza mechi 23.