MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameendelea kuthibitisha ubora wao katika ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa nane mfululizo kufuatia kuwachapa Maafande wa JKT Tanzania mabao 5-0, mechi iliyopigwa leo Jumatano Februari 25, 2026 kwenye Uwanja wa KMC, Dar.
Ushindi huo mnono unaifanya Yanga kama kutuma salamu kuelekea kwenye Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba, huku ikiwa kifua mbele huku ikikaa kileleni mwa msimamo wa ligi.
Tangu dakika za mwanzo za mechi hiyo, Yanga ilionesha kiu ya ushindi kwa kulishambulia lango la JKT. Dakika ya saba tu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliwainua mashabiki baada ya kufunga bao la mapema akimalizia pasi safi ya Prince Dube. Bao hilo liliwapa utulivu na kujiamini wachezaji wa Yanga, ambao waliendelea kumiliki mpira na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga.
Laurindo Dilson ‘Depu’ alipata nafasi nzuri kipindi cha kwanza lakini shuti lake liliokolewa na kipa Ramadhan Chalamanda. JKT nayo ilijaribu kujibu mashambulizi na dakika ya 41, Paul Peter aliachia mkwaju ambao uliokolewa na Djigui Diarra, hivyo Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuongeza kasi na kufanya mabadiliko madogo kwa kuingia Mohamed Damaro na kutolewa Allan Okello, mabadiliko hayo yaliimarisha eneo la kiungo. Mudathir Yahya alianza kuonekana zaidi katika mashambulizi, akiunganisha safu ya kati na ushambuliaji.
Dakika ya 61, Depu alipachika bao la pili kwa kichwa, likiwa ni bao lake la tano msimu huu katika ligi hiyo. Dakika mbili baadaye, Mudathir Yahya aliongeza la tatu na kuzidi kuwakatisha tamaa maafande hao.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alitumia nafasi hiyo kuwapumzisha baadhi ya nyota wake, lakini kasi ya timu haikupungua. Dakika ya 85, Prince Dube alifunga bao la nne kabla ya Shekhani Khamis kuhitimisha ushindi huo kwa bao la tano.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 28, sawa na JKT Tanzania lakini imekaa kileleni kwa tofauti ya mabao. Yanga imecheza mechi kumi, JKT Tanzania ikifikisha mechi 17.
Tangu ilipotoka sare ya 0-0 dhidi ya Mbeya City Septemba 30, 2025, Yanga imeshinda mechi nane mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0), KMC (4-1), Fountain Gate (2-0), Coastal Union (1-0), Mashujaa (6-0), Dodoma Jiji (3-1), Namungo (1-0) na JKT Tanzania (5-0).
Jumapili Machi Mosi 2026, Yanga itaikaribisha Simba katika Dabi ya Kariakoo ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Yanga; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohammed Hussein, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Mudathir Yahya, Max Nzengeli, Allan Okello, Laurindo Dilson ‘Depu’, Prince Dube na Duke Abuya.
JKT Tanzania; Ramadhan Chalamanda, Anuary Kilemile, Karimu Mfaume, Hassan Nassor, Sospeter Bajana, Salehe Karabaka, Edson Katanga,Ally Msengi, Paschal Mussa, Paul Peter na Mohamed Bakari.