Katika utafiti wake mpya unaoitwa ”Uhalifu na usafirishaji haramu wa Taka” , ambao ni sehemu ya uchambuzi wa kimataifa kuhusu uhalifu unaoathiri mazingira, UNODC inaonya kuwa mitandao ya uhalifu pamoja na baadhi ya makampuni yanatumia mianya ya kisheria na udhaifu wa utekelezaji wa sheria kusafirisha taka hatarishi kuvuka mipaka na mara nyingi kuelekea nchi zenye kipato cha chini ambazo hazina uwezo wa kuzisimamia kwa usalama taka hizo.
Wachambuzi wa ripoti wanasema mapungufu ya sheria, adhabu ndogo na ukosefu wa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji vimeifanya biashara hiyo kuwa soko haramu linalokadiriwa kuingiza mabilioni ya dola.
Soko la taka za kielektroniki Bankok Thailand
Changamoto ni kubwa na ya kutisha
Mkurugenzi wa Uchambuzi wa Sera na Masuala ya Umma wa UNODC, Candice Welsch, anasema changamoto hiyo ni kubwa na ya kutisha.
“Utafiti wetu unaonesha kuwa biashara haramu ya taka bado ni vigumu sana kugundua, kuchunguza na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria,” amesema. “Hili si suala la kinadharia, bali lina madhara makubwa kwa afya ya umma, kwani linachochea uchafuzi wa sumu katika maji ya kunywa, bahari, udongo na maeneo mengine.”
Ripoti hiyo pia imebaini kuwa makundi ya uhalifu wa kupangwa yanafanya kazi katika ngazi za ndani na za kimataifa, yakificha taka haramu ndani ya mizigo halali kupitia udanganyifu wa nyaraka, rushwa na utakatishaji fedha.
Wakati mwingine, baadhi ya makampuni hununua kwa makusudi huduma haramu za utupaji taka au kuendesha shughuli haramu sambamba na zile halali.
Bi Welsch anasisitiza haja ya ushirikiano wa karibu zaidi wa kimataifa. “Kuboresha mawasiliano na takwimu kuhusu njia zinazotiliwa shaka na mianya katika mnyororo wa biashara ya taka, pamoja na kuoanisha makosa na adhabu, ni muhimu ili kutabiri, kuzuia na kusitisha mtiririko wa taka haramu.”
UNODC inaonya kuwa taka nyingi husafirishwa kutoka nchi zenye kipato cha juu kwenda nchi zenye kipato cha chini, hasa plastiki na taka za kielektroniki zenye kemikali hatarishi.
Imeongeza kuwa kwa kuwa adhabu mara nyingi ni ndogo kuliko faida inayoweza kupatikana, wahalifu huchagua nchi zenye sheria dhaifu zaidi na kuziacha jamii zilizo hatarini zikibeba mzigo wa sumu hiyo.