Kigoma. Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) imesaini mkataba wa ushirikiano na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kudhibiti rasilimali za maji, kilimo, sekta ya uchukuzi, kuunganisha shughuli za kiuchumi na maisha ya watu wanaozungukwa na maziwa hayo.

Akizungumza leo Februari 25, 2026 mjini Kigoma, baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mtendaji wa LVBC, Masinde Bwire amesema mkataba huo ni muhimu, kwani maziwa hayo mawili yamekuwa yakitegemewa sana kwa usafirishaji wa mizigo ndani ya Tanzania na nchi jirani, hivyo kuongeza ushirikiano wa kibiashara kikanda.

“Mkataba huu ni muhimu tukumbuke kuwa ziwa Tanganyika ndiyo ziwa la pili kwa kuwa na kina kirefu duniani na la pili duniani kuwa na ujazo mkubwa wa maji likiwa na takribani asilimia 17 ya ujazo wa maji duniani na kilomita za ujazo 18,900 ina maana lina maji mengi mara saba zaidi ya maji ya ziwa Victoria lenye jumla ya maji ya kunywa zaidi ya ujazo wa kilomita 2,800,” amesema Bwire.

Amesema kwenye kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kudhibiti rasilimali za maji, watajikita kwenye utunzaji wa rasilimali za maji, usalama na uchukuzi majini, utunzaji wa mazingira na maliasili, lengo ni kuhakikisha rasilimali hizi zinaendelea kuwanufaisha watu wa mataifa yote wanaozunguka maziwa hayo.

Bwire amesema ni muhimu wananchi wanazungukwa na maziwa hayo kutunza vyanzo vya maji na kuacha kuchafua kwa kutupa taka na shughuli nyingine za kibinadamu ambazo si salama kwa rasilimali hizo, kwani inachukua hadi miaka 7,000 kwa ziwa kujisafisha ambapo ni sawa na karne 7.

“Tuna changamoto zinazofanana kwa upande wa maziwa yote mawili, yaani ziwa Tanganyika na Victoria hivyo lazima tuwe na mipango ya pamoja kuweza kukabiliana kimkakati na changamoto hizo, hivyo tukiunganisha nguvu kwa pamoja tutaweza kutatua na kuwa bora zaidi kwa eneo lote la ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini,” amesema Bwire

Mkurugenzi Mtendaji wa LTA, Tusanga Sylvain amesema ziwa Tanganyika lina changamoto mbalimbali ikiwemo ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na hasa na taka za plastiki, hivyo wakiungana kwa pamoja wanaweza kuzitatua kwa kupunguza au kumaliza kabisa changamoto hizo.

Sylvain amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maziwa hayo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Baadhi ya wananchi wamesema pamoja na kusaini kwa mkataba wa ushirikiano wa kufanya kazi ni muhimu wakawekeza pia katika suala la utoaji wa elimu kwa wananchi, ili iwe rahisi wao wenyewe kuwa wa kwanza katika utunzaji wa rasilimali hizo.

“Wananchi wamekuwa wakilima karibu na vyanzo vya maji, uvuvi haramu una uchafuzi wa namna nyingi ndani ya ziwa hilo, kama hawana elimu ya jinsi ya kutunza na umuhimu wake kwao na vizazi vijavyo itakuwa ni kazi bure hivyo kuwashirikisha wananchi kwenye utunzaji huo kutakuwa na matokeo chanya,” amesema Bahati Samweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *