Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya fasheni na urembo duniani imeonesha mabadiliko makubwa, ambayo yamekuwa yakiwavutia watu mbalimbali. 

Tofauti na zamani maonesho ya mitindo na matangazo ya bidhaa yalitawaliwa zaidi na sura za aina moja. Lakini kwasasa soko hili limetawaliwa zaidi na models weusi ambao wamekuwa sehemu muhimu ya kampeni katika chapa kubwa kimataifa.

Jarida la mitindo la kimataifa Vogue limefichua siri ya ongezeko la models weusi kwenye runway na matangazo mbalimbali. Limeeleza kuwa moja ya sababu ni tasnia ya fasheni kuendana na dunia halisi ambayo haibagui rangi wala tamaduni. Huku wakitaja mchango wa supermodel Naomi Campbell, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akipigania usawa katika fasheni.

Aidha kwa mujibu wa The Business of Fashion, inaeleza chapa nyingi zimegundua kuwa utofauti wa rangi ‘Diversity’ si suala la kijamii pekee bali ni mkakati wa kibiashara. Uchunguzi huo unaonesha kuwa watu weusi wananguvu kubwa katika masoko ya kibiashara. Hivyo chapa hutafuta models wanaoweza kuwakilisha wateja hao moja kwa moja.

Nalo gazeti la Marekani, The New York Times liliwahi kufanya mahojiano na wakurugenzi wa chapa mbalimbali. Ambapo walieleza kuwa sababu kubwa ya kutumia models weusi ni kutokana na mabadiliko ya kizazi cha sasa kuthamini watu weusi. Huku kampuni mbalimbali za vipodozi zilivyoanza kuzalisha rangi nyingi za foundation ili kukidhi mahitaji ya ngozi tofauti, hasa ngozi nyeusi.

Hata hivyo Jarida la biashara Forbes liliongeza kwa kueleza kampeni au matangazo ambayo yanamchanganyiko wa rangi kwa wahusika wake zimekuwa zikipata wafuatiliaji wengi mitandaoni. Jambo ambalo limekuwa likiongeza mauzo na uaminifu kwa wateja hasa kwa kizazi cha sasa ‘Gen Z’.

Wanamitindo weusi wanaotamba kwenye maonyesho makubwa na kampeni za chapa za kifahari ni Adut Akech, Anok Yai, Duckie Thot, Winnie Harlow, Jourdan Dunn pamoja na Alek Wek.

Aidha kwa nyakati tofauti models hao wamekuwa wakifichua namna mafanikio yao yalivyokuja. Ambapo wanaeleza kwa miaka mingi nafasi zilikuwa chache kwa models wenye ngozi nyeusi, lakini kadri jamii ilivyoanza kuthamini utofauti, chapa kubwa zimegundua kuwa rangi na muonekano wao huwavutia wateja wengi zaidi.
    

Pia wanaamini mitandao ya kijamii imewapa nguvu ya kujionesha moja kwa moja kwa hadhira ya kimataifa bila kutegemea mifumo ya zamani ya fasheni. Hali iliyosaidia kubadili sheria za awali zilizokuwa zikiwabana.

Kwao kuongezeka kwa models weusi si bahati bali ni matokeo ya mabadiliko ya soko. Ambapo wateja wanataka kuona wakiwakilishwa na watu tofauti ambao wananguvu katika soko la kibiashara katika tasnia ya mitindo duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *