
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya maeneo vituo vya nyuklia vya Iran ya mwezi Juni mwaka huu, ni “sura ya giza na hatari” katika historia ya Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo wakati wa mkutano na mawaziri wenzake wa Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas mjini New York. Araqchi yuko nchini Marekani kuhudhuria kikao cha 80 cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Amesema, hayo yalikuwa ni mashambulizi ya kihalifu ambayo yalifanywa kama sehemu ya vita vilivyoanzishwa na Tel Aviv na Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuanzia Juni 13 hadi Juni 25, 2025. Mbali na kulengwa vituo hivyo, vita hivyo vilipoteza maisha ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran pamoja na makamanda wakuu wa kijeshi na raia wa kawaida, wakiwemo watoto wadogo.
Mkutano huo ulifanyika kama sehemu ya mazungumzo kati ya Iran na wawakilishi wa mataifa ya Ulaya yanayojulikana kwa jina la Troika ya Ulaya ambayo yanawakilisha mataifa ya Magharibi na washirika wao katika kadhia ya nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.
Waziri Araqchi ameashiria pia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kama sehemu ya juhudi za kuonesha nia njema Iran katika mradi wake wa amani wa nyuklia na kusema kuwa, haijawahi kuthibitishwa hata mara moja kwamba shughuli za nyukliaza Iran zimetoka kwenye msingi wake wa amani.