Nyota wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, ameanza rasmi safari ya kuelekea kustaafu soka baada ya kununua asilimia 25 ya hisa katika klabu ya daraja la pili Hispania, UD Almería hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya maisha baada ya kustaafu uwanjani.
Uamuzi huo unakuja wakati mshambuliaji huyo wa Al Nassr na nahodha wa Ureno akikaribia mwisho wake kwenye soka akiacha historia ndefu katika miongo miwili aliyodumu uwanjani.
Ronaldo, ambaye aliwahi kutamba kwa mafanikio makubwa akiwa Real Madrid kati ya 2009–2018, amekuwa akisema kwa miaka kadhaa kuwa angependa kumiliki klabu baada ya kustaafu.
Mshambuliaji wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo akishangilia moja ya bao alilofunga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Saudia Pro. Picha na Mtandao
Sasa kupitia kampuni yake ya uwekezaji ya CR7 Sports Investments, ndoto hiyo imeanza kutimia baada ya kununua hisa Almeria.
“Ni ndoto yangu ya muda mrefu kuchangia soka nje ya uwanja,” alinukuliwa akisema baada ya uwekezaji huo.
Hatua hiyo pia inaashiria kurejea kwake katika soka la Hispania, alikoacha rekodi na mataji mengi kabla ya kuhamia Juventus mwaka 2018.
Wachezaji wa Klabu ya Almeria inayoshikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ya Segunda División wakishangilia. Picha na Mtandao
Mshindi huyo wa Ballon d’Or mara tano tayari amethibitisha kuwa Kombe la Dunia lijalo litakuwa la mwisho kwake kimataifa.
Akiwa na umri wa zaidi ya miaka 40, Ronaldo mwenyewe amekiri kuwa amebakiwa na mwaka mmoja au miwili tu ya kucheza soka.
Cristiano Ronaldo ni mshindi mara tano wa tuzo za Ballon d’Or. Picha na Mtandao
Wachambuzi wamepongeza uwekezaji wa nyota huyo katika klabu ya Almeria wakiutaja kama mpango mahsusi wa kujihakikishia nafasi ndani ya soka hata baada ya kutundika daluga tofauti na mastaa wengi wanaochagua ukocha au uchambuzi.
Njia ya Beckham na Mbappé
Hatua ya Ronaldo inaiga nyayo za mastaa wachache waliogeukia umiliki wa klabu, akiwamo David Beckham ambaye anamiliki Inter Miami ya Marekani, pamoja na Kylian Mbappé mwenye hisa kubwa katika SM Caen ya Ufaransa.
Aidha, Ronaldo ndiye mwanasoka anayelipwa zaidi kuwahi kutokea, akipokea mshahara unaokadiriwa Pauni milioni 177 kwa mwaka Saudi Arabia (zaidi ya Sh6 bilioni).
Tathmini za kifedha zinaonyesha thamani ya mali zake imevuka Pauni bilioni 1 (zaidi ya Sh3 trilioni), kutokana na mishahara, matangazo na uwekezaji.
Mmiliki wa hisa asilimia 25 katika klabu ya UD Almeria, Cristiano Ronaldo akisaini mkataba. Picha na Mtandao
Ana mkataba wa kudumu na kampuni ya michezo Nike unaokadiriwa kufikia thamani ya dola za Marekani bilioni moja (zaidi ya Sh trilioni 2.5), pamoja na ushirikiano na chapa kubwa duniani.
Mbali na klabu, Ronaldo ana mtandao mpana wa uwekezaji na mali ambapo ana majengo ya kifahari nchini Ureno, ikiwamo jumba kubwa Quinta da Marinha, Hoteli za CR7 katika miji mbalimbali duniani.
Pia, ana biashara ya mitindo na manukato (CR7 brand), kampuni ya uzalishaji wa vifaa na afya/fitness na uwekezaji katika teknolojia na michezo.
Cristiano Ronaldo akiwa amekalia moja ya gari lake aina ya Bentley. Picha na Mtandao
Maisha ya kifahari ya staa huyo yanaonekana kuendelea hata baada ya soka, akijenga kile kinachoelezwa kuwa moja ya nyumba ghali zaidi Ureno yenye bwawa la kioo na vyumba vikubwa vya kifalme.
Maono yake United
Ronaldo amewahi kusema hata angependa siku moja kumiliki klabu aliyochezea zamani, hasa Manchester United, akisisitiza kuwa matatizo ya klabu hiyo yanahitaji mageuzi ya uongozi.
“Kama ningekuwa mmiliki, ningerekebisha mambo mabaya,” aliwahi kusema.