
Dar es Salaam. Kuteuliwa kwa Nassoro Mwinchui kuchezesha mechi ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba, Jumapili, Machi Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kunamaliza historia ya miaka mitano na miezi minne inayowahusu marefa katika mechi za igi baina ya timu hizo.
Leo, Ijumaa, Februari 27, 2026, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemntangaza Mwinchui kuwa ndio atakuwa refa wa kati akisaidiwa na Kassim Mpanga na Hamdani Said huku refa wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mwinchui kutoka Tanga, kuchezesha mechi baina ya timu hizo mbii katika mashindano tofauti hapa nchini.
Ukiondoa kuchezesha kwa mara ya kwanza mechi ya Watani wa Jadi kwenye Ligi Kuu, Mwinchui anakuwa refa wa kwanza asiye na beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kusimama katikati katika mchezo wa Ligi Kuu wa Dabi ya Kariakoo baada ya kipindi cha miaka mitatu na miezi 11 kupita.
Mara ya mwisho kwa refa asiye na beji ya FIFA kuchezesha mechi ya igi Kuu baina ya Yanga na Simba ilikuwa ni Julai 3, 2021 ambapo timu hizo zilichezeshwa na Emmanuel Mwandembwa ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Baada ya hapo, mechi nane zilizofuata zilichezeshwa na marefa ambao walikuwa na beji za FIFA.
Desemba 11, 2011, timu hizo ziichezeshwa na Hery Sasii na kutoka sare ya 0-0 na Aprili 30, 2022 zikatoka tena sare tasa pindi zilipochezeshwa na Ramadhan Kayoko.
Oktoba 23, 2022, Kayoko alizichezesha tena na zikatoka sare ya bao 1-1 na katika marudiano, Aprili 16, 2023, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku refa akiwa ni Jonesia Rukyaa.
Ahmed Arajiga alisimama katikati, Novemba 5, 2023 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 na ziliporudiana tena Aprili 20, 2024 Arajiga akashika tena filimbi na Simba ikapoteza kwa mabao 2-1.
Msimu uiopita, mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Oktoba 19, 2024, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, refa akiwa ni Ramadhan Kayoko na ziliporudiana Juni 25, 2025, refa kutoka Misri, Mohamed Amin alisimama katikati na Simba ikafungwa mabao 2-0.
Ikumbukwe mwaka huu, Tanzania ina marefa sita wa kati wenye beji za FIFA ambao watano wanatoka Tanzania Bara na mmoja Zanzibar.
Marefa wa kati wenye beji za FIFA wa Tanzania Bara ni Arajiga, Kayoko, Sasii, Amina Kyando na Tatu Malogo huku kutoka Zanzibar akiwa ni Nasir Siyah.