
Kwimba. Wahudumu wa afya wanaotarajia kutoa huduma katika jengo jipya la watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, wamepatiwa mafunzo maalum ya matumizi ya vifaa vya kisasa na mbinu bora za kuwahudumia watoto wachanga njiti na mama zao ili kuboresha huduma na kupunguza rufaa zisizo za lazima.
Mafunzo hayo yameendeshwa na wataalamu wa afya ya mtoto yakihusisha wahudumu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na vituo vya afya vyenye mzigo mkubwa wa wagonjwa katika wilaya za Kwimba na Misungwi, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa huduma katika jengo hilo jipya la watoto wachanga.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wachanga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Daktari Bingwa Mbobezi wa Watoto Wachanga, Dk Martha Mkony, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka wakati hospitali hiyo ikijiandaa kufungua jengo maalum la huduma za watoto wachanga.
Amesema washiriki wanapewa elimu ya nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo wa kutumia vifaa vya kisasa na kutoa huduma salama kabla ya kukabiliana na wagonjwa, akibainisha kuwa wodi hiyo ni ya kwanza nchini kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Mafunzo haya yamegusa huduma za mama na mtoto na yanakwenda sambamba na juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha afya ya watoto wachanga nchini,” amesema.
Kwa upande wake, mhudumu wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Elizabeth Honela, amesema elimu waliyopata ikiwamo dhana ya ‘zero separation’ kati ya mama na mtoto itasaidia kuboresha huduma kwa watoto njiti na kupunguza vifo na rufaa.
Amesema kupatikana kwa jengo jipya la watoto njiti lililojengwa na Doris Mollel Foundation lenye vifaa tiba vya kisasa kutasaidia hospitali hiyo kuhudumia watoto wengi zaidi tofauti na awali ambapo walilazimika kuwapeleka rufaa.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Doris Mollel Foundation kwa ushirikiano na World Health Organization (WHO) huku wauguzi walioshiriki wakitolewa na Serikali kupitia wizara ya afya.