Chanzo cha picha, EPA
-
- Author, Yolande Nell
- Nafasi, Ripota wa Mashariki ya kati, Ramallah
-
Muda wa kusoma: Dakika 6
Kadri vurugu za walowezi wa Kiyahudi wa Israel zinavyozidi kuongezeka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kijiji cha Mughiyar, kaskazini-mashariki mwa Ramallah, kimekuwa kitovu cha mvutano. Kijiji hicho kimekuwa kikilengwa na uvamizi wa jeshi la Israel na kushuhudia ardhi za kilimo zikichukuliwa na walowezi walioanzisha maeneo mapya ya makazi.
Marzouk Abu Naim wa baraza la kijiji cha Mughiyar anasema lengo la walowezi ni kuwafukuza Wapalestina. “Wanafanya kimya kimya, si kwa wazi,” anasema. “Lakini lengo ni kunyakua ardhi. Hatuwezi tena kufikia mashamba yetu.”
Kijiji cha Mughiyar kimezungukwa na vilima vya kijani na mashamba ya mizeituni. Nyumba nyingi ziko katika eneo linalodhibitiwa kiusalama na jeshi la Israel, lakini kwa mujibu wa makubaliano, Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono kimataifa ilipaswa kutoa huduma za msingi. Hata hivyo, taasisi hiyo sasa imeshindwa kufanya hivyo kutokana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaozidi kuongezeka.
“Nikienda kwao, hawawezi kunipa msaada ninaohitaji,” anasema Abu Naim. “Taasisi haina fedha!”.
Baada ya mashambulizi mabaya yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, takriban Wapalestina 100,000 walipoteza vibali vyao vya kufanya kazi Israel.
Aidha, Israel imesitisha uhamishaji wa mapato ya kodi inayokusanya kwa niaba ya Mamlaka hiyo, kufuatia mvutano kuhusu maudhui ya vitabu vya shule vya Kipalestina na malipo ya posho kwa familia za waliofungwa au kuuawa na Israel, wakiwamo washambuliaji.
Mamlaka ya Palestina inasema sasa inaidai Israel zaidi ya dola bilioni 4. Inawalipa wafanyakazi wengi wa sekta ya umma, wakiwamo madaktari, polisi na walimu, asilimia 60 tu ya mishahara yao. Shule zinazoendeshwa na Mamlaka hiyo, zinazohudumia zaidi ya wanafunzi 600,000, hufunguliwa siku tatu tu kwa wiki.
“Ni vigumu sana,” anasema mama wa watoto wanane kutoka Mughiyar, akieleza kuwa shule hufungwa pia walowezi au wanajeshi wanapokuwapo, kwa hofu ya usalama wa watoto.
Anaongeza: “Pengo la elimu limekuwa kubwa kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi wa darasa la nne bado hawajui kusoma. Tunalazimika kuwapeleka katika darasa la awali la binafsi kijijini waanze tena na alfabeti.”
Chanzo cha picha, EPA
Njiani kutoka Mughiyar, vituo vya kijeshi vya Israel vinaonekana, vikizuia mawasiliano kati ya vijiji vya Kipalestina na kudhibiti harakati.
Mitambo ya kubomoa ya Israel pia inapanua barabara ili kuunganisha makazi ya walowezi na kuwapa njia ya haraka kuelekea Jerusalem.
Makazi hayo, yanayochukuliwa kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa, yanaendelea kupanuka kwa kasi isiyokuwa ya kawaida.
Hali hii imeongeza shinikizo kwa Mamlaka ya Palestina, iliyoanzishwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kufuatia Makubaliano ya Oslo.
Wapalestina walitarajia kuwa Mamlaka hiyo ingegeuka haraka kuwa serikali kamili ya dola huru ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, huku Jerusalem Mashariki ikiwa mji mkuu. Iliahidi kufikia lengo hilo kupitia mazungumzo na njia zisizo za vurugu.
Hata hivyo, mazungumzo ya moja kwa moja na Israel yalivunjika zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Kushindwa kwa Mamlaka kuzuia upanuzi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi-achilia mbali kuanzisha dola huru—kumeweka wazi udhaifu wake na kuongeza hasira za wananchi dhidi ya rushwa, mkwamo wa kisiasa na ushirikiano wa kiusalama na Israel.
Ninafuata msururu mrefu wa magari yanayongoja kupitia kituo cha ukaguzi cha jeshi la Israel hadi Ramallah, kituo kikuu cha utawala cha Mamlaka ya Palestina. Polisi wa Palestina wako mitaani. Hii ni sehemu ya Ukingo wa Magharibi ambayo Mamlaka bado ina udhibiti kamili juu yake.
Onyo kuhusu kusambaratika kwa taasisi hiyo linaongezeka.
“Hii ni hatua ya mabadiliko makubwa katika maisha yetu,” anasema Sabri Saidam, aliyekuwa waziri wa Mamlaka hiyo. “Dola ya Palestina, utambulisho wa Kipalestina, na hata uwepo wa Wapalestina katika ardhi yao ya asili sasa uko hatarini.”
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi Februari, serikali ya Israel ilichukua hatua mpya za kuimarisha udhibiti wake katika Ukingo wa Magharibi, huku afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa akionya kuwa hatua hizo zinakaribia kuwa “unyakuzi wa taratibu na wa vitendo.”
Mchakato mpya wa usajili wa ardhi unaweza kuruhusu Israeli kusajili maeneo makubwa ya ardhi kama ardhi ya taifa la Israeli kwa maendeleo ya siku zijazo, na utekelezaji wa kanuni za mazingira na kiakiolojia za Israeli umepanuliwa hadi sehemu za Ukingo wa Magharibi chini ya udhibiti wa raia.
Katika mkutano katika mji karibu na Ramallah, Waziri wa Fedha wa Israel mwenye misimamo mikali, Bezalel Smotrich, ameahidi kufuta rasmi Makubaliano ya Oslo na kuivunja Mamlaka ya Palestina iwapo ataendelea kuwa serikalini baada ya uchaguzi wa 2026.
Zaidi ya nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, zimelaani hatua za upande mmoja za Israel. Marekani imerudia tu kupinga unyakuzi wa Ukingo wa Magharibi.
Wapalestina wengi wana wasiwasi na kukata tamaa. Ghassan Khatib, profesa wa masomo ya kimataifa, ametoa wito wa shinikizo la kimataifa kwa Israel na usaidizi wa kifedha ili kuhakikisha uhai wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
“Hii inapaswa kuwa ari ya kuamsha,” ananiambia. “Ulimwengu wa nje umewekeza sana kisiasa na kifedha katika wazo la suluhisho la serikali mbili, lakini hatua hizi mpya za Israeli zinalenga kuharibu mustakabali wa suluhisho hilo.”
Chanzo cha picha, EPA
Wakati huo huo, vita vinavyoendelea Gaza vimeharakisha kudhoofika kwa Mamlaka hiyo, ambayo ilipoteza udhibiti wa eneo hilo mwaka 2007 baada ya Hamas kushinda uchaguzi wa bunge.
PA ilichelewa kulaani mashambulizi mabaya ya Hamas dhidi ya Israel ambayo yalichochea vita, na sasa imetengwa kwa kiasi kikubwa katika utawala wa baada ya vita kwa amri ya Israel.
Tofauti na Israel, Mamlaka ya Palestina si mwanachama wa “tume ya amani” inayoongozwa na Marekani. Hata hivyo, inatarajiwa kufuatilia karibu vikosi 5,000 vya polisi huko Gaza.
Mpango wa amani wa Donald Trump pia unatazamia kwamba tume hatimaye itadhibiti eneo hilo baada ya kukamilisha “mpango wa mageuzi” ambao haujaainishwa, unaoashiria mustakabali ambapo “masharti yapo kwa njia ya kuaminika kuelekea kujitawala na kuanzishwa kwa taifa la Palestina”.
Viongozi wa Israel wamekataa mapendekezo kwamba Mamlaka hiyo inakaribia kusambaratika, jambo ambalo litailazimisha Israel, kama mamlaka inayokalia, kuwajibika moja kwa moja kwa takriban Wapalestina milioni 2.7 wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi.
Afisa wa serikali ya Israel aliiambia BBC: “Mamlaka ya Palestina ni taasisi fisadi na iliyofilisika kimaadili ambapo rasilimali kubwa zimeporwa badala ya kuwafikia watu wake.”
Katika kijiji cha Mughiyar, walowezi tayari wamewafukuza wafugaji wa Bedouin na sasa wanachunga mifugo yao karibu na kambi mpya. Wanajeshi wa Israel wanaendelea kushika doria, huku mabomu ya machozi yakirushwa mara kwa mara.
Haya yanajiri, mwezi mmoja baada ya Mpalestina mwenye umri wa miaka 14 kupigwa risasi na mwanajeshi wa Israel hapa. Jeshi linasema alikuwa akirusha mawe. Katika kesi hiyo pia, jeshi lilisema mawe yalirushiwa askari wake na watuhumiwa walikamatwa.
Ingawa kuna umakini mdogo wa kimataifa kwa hali halisi ya kila siku ya Ukingo wa Magharibi, wakaazi wanasema hatari ya machafuko yaliyoenea inaongezeka. Kuna hofu kwamba kudhoofika kwa Mamlaka ya Palestina kunaweza kuwasukuma baadhi ya Wapalestina kuelekea makundi yenye misimamo mikali zaidi.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid