Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa utawala wa Iran “haupaswi kumiliki silaha za nyuklia” kwa kuwa ni tishio kwa usalama wa Israel na dunia.
Akihutubia wananchi wa Israel, Netanyahu alisema:
“Enyi ndugu zangu, raia wa Israel, muda mfupi uliopita, Israel na Marekani zilianza operesheni ya kuondoa tishio la moja kwa moja linalotokana na utawala wa kigaidi wa Iran.”
Alimshukuru Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kile alichokiita uongozi wa kihistoria, akisema kwa miaka 47 utawala wa Ayatollah umekuwa ukipaza sauti kauli za “Kifo kwa Israel” na “Kifo kwa Marekani.”
Amedai kuwa utawala huo umehusika na umwagaji damu wa Waisraeli, vifo vya Wamarekani na ukandamizaji wa raia wake wenyewe, akiongeza kuwa:
“Utawala huu wa kigaidi na wauaji haupaswi kupewa silaha za nyuklia ambazo zingeuruhusu kutishia ubinadamu wote.”
Netanyahu alisema hatua ya pamoja ya Israel na Marekani italeta mazingira yatakayowawezesha wananchi wa Iran “kuchukua hatima yao mikononi mwao.”
Alitoa wito kwa makundi mbalimbali ya wananchi wa Iran, Waajemi, Wakurdi, Waazeri, Wabaluchi na Waahwazi, kuondokana na kile alichokiita nira ya udikteta na kuijenga Iran huru na yenye amani.
Kwa wananchi wa Israel, aliwataka kufuata maelekezo ya Kamandi ya Ulinzi wa Ndani, akisema katika siku zijazo za operesheni iliyopewa jina la “Mngurumo wa Simba,” taifa litahitaji uvumilivu na uthabiti.
“Pamoja tutasimama, pamoja tutapigana, na pamoja tutahakikisha kudumu kwa Israel,” alisema.