DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Bunge Marathon na Bunge Bonanza, Festo Sanga, ametangaza kuwa mbio za Bunge Marathon msimu wa tatu zinatarajiwa kufanyika Aprili 18, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Sanga amesema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika na lengo kuu ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhamasisha michezo na mazoezi nchini.

Amesema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuonesha kwa vitendo umuhimu wa mazoezi na kuunga mkono wanamichezo, ikiwemo kuzisaidia timu za taifa na klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

“Sisi kama wabunge tumeamua kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake katika kusimamia michezo nchini. Tunatambua pia kuwa tunawawakilisha wananchi, hivyo tumeona ni vyema kushirikiana nao kupitia michezo. Ndiyo maana tumekuja na kauli mbiu isemayo; ‘Ewe mwananchi njoo ukimbie na mbunge wako’,” amesema Sanga.

Ameeleza kuwa mbio hizo zitahusisha kilomita 5, 10 na 21, na kwamba ni marathon ya kimataifa iliyokidhi viwango vinavyotakiwa. Amesisitiza kuwa ni marathon ya kila Mtanzania na usajili umefunguliwa rasmi kuanzia Februari 28, 2026 kwa gharama ya Sh 40,000 kupitia mfumo maalum wa mtandaoni uliotengwa kwa ajili hiyo.

Kwa mujibu wa Sanga, katika misimu iliyopita zaidi ya washiriki 5,000 walishiriki, huku waandaaji wakilenga kuvunja rekodi mwaka huu kwa kuongeza idadi ya washiriki, wakiwemo wanariadha kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Silent  Ocean, Mohamed Soloka, ambao ni wadhamini wa mbio hizo, ameahidi kutoa vifaa bora na vya kisasa vitakavyotumika katika mashindano hayo. Amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki, akisema udhamini huo unatokana na imani yao kuwa Bunge ni mhimili muhimu wa taifa.

“Tumedhamini Bunge Marathon kwa sababu huu ni mhimili wa taifa. Tunaamini ushirikiano huu utanufaisha pande zote na mwaka huu Bunge Marathon itakuwa ya kihistoria,” amesema Soloka.

Mbali na mashindano, Bunge Marathon pia itatumika kama jukwaa la kuchangia damu salama kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa damu kwa wananchi wenye uhitaji.

Washindi watatu wa kwanza katika kila mbio watajishindia zawadi za fedha taslimu. Katika kilomita 5, mshindi wa kwanza atapata Sh 2,000,000, wa pili Sh 1,000,000 na wa tatu Sh 500,000. Kwa kilomita 10, mshindi wa kwanza atapata Sh3,000,000, wa pili Sh 2,000,000 na wa tatu Sh 1,000,000. Katika kilomita 21, mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh 6,000,000, wa pili Sh 3,000,000 na wa tatu Sh1,500,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *