Mwanza. Vijana 336 kati ya 400 waliopatiwa mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi wa Vijana Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) wametunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo yao, huku wakikabidhiwa vifaa vya kuanzia kazi vyenye thamani ya Sh69 milioni kulingana na fani walizosomea.
Katika utekelezaji wa mradi huo, zaidi ya Sh160 milioni zimetumika kulipia ada za mafunzo na kununua vifaa vya kujifunzia kwa vijana hao, waliopata mafunzo kupitia chuo vya VETA mkoani Mwanza.
Mradi huo unatekelezwa na Plan International kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (DGD), ukilenga kuwawezesha vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika mahafali yaliyofanyika leo Februari 27, 2026 jijini Mwanza, Mratibu wa mradi huo, Gadiel Kayanda amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana kutoka mazingira magumu kujikwamua kiuchumi.
“Hawa ni vijana tuliowatambua kupitia jamii wakiwa katika mazingira magumu. Wengine walikatisha masomo kutokana na mimba za utotoni, wengine walishindwa kuendelea na elimu ya juu. Tuliona ni muhimu kuwapa mwelekeo mpya,” amesema Kayanda.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi wa VEMA.
Amesema kati ya wahitimu hao, wanaume ni 135 na wanawake 211, hatua inayolenga kukuza usawa wa kijinsia katika fursa za mafunzo na ajira.
Kayanda amewataka vijana hao kutumia ujuzi walioupata kujiletea maendeleo badala ya kuuweka bila kuutumia kwakuwa wakikaa nao bila kuufanyia kazi itakuwa sawa na kutokusoma kabisa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa amewaonya wahitimu dhidi ya kuuza vifaa walivyokabidhiwa kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji.
“Hatutarajii kuona vifaa hivi vinauzwa. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo,” amesema Mkalipa.
Aidha, amewahamasisha vijana kuunda vikundi na kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya vijana, wanawake na wazee.
Mradi huo pia umefanikiwa kuunda vikundi 53 vya kuweka na kukopa (VSLA), ambapo vijana wamepatiwa mafunzo ya elimu ya fedha, biashara, ujasiriamali, usawa wa kijinsia na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
Hadi sasa vikundi hivyo vimeweka akiba ya zaidi ya Sh200 milioni ambapo zaidi ya Sh110 milioni zimetolewa kama mikopo kwa wanachama kuanzisha na kuendeleza biashara ndogondogo.
Pamoja na mafanikio hayo, Kayanda amesema changamoto zilizojitokeza ni pamoja na utoro wa baadhi ya wanafunzi, baadhi ya wazazi au walezi kuwazuia vijana kushiriki mafunzo, pamoja na mabadiliko ya haraka ya matarajio ya vijana kulingana na hali ya kijamii na kiuchumi.
Mradi huo unalenga kufikia vijana 800 mkoani Mwanza kwa kuwapatia elimu, kukuza usawa wa kijinsia na kuwafungulia fursa za ajira na ujasiriamali.
Baadhi ya wahitimu wameeleza kufurahishwa na matokeo ya mradi huo wakisema mafunzo hayo yamewapa dira mpya ya maisha.
“Naenda kuanzisha shughuli itakayoniwezesha kujiendeleza kiuchumi, ninaamini nitasonga mbele,” amesema Ester Cheni,
Naye Kelvin Daniel amesema ujuzi alioupata utamwezesha kujiajiri bila kusubiri ajira serikalini au sekta binafsi.
“Tutumie elimu tuliyoipata kujitengenezea kipato badala ya kulaumu ukosefu wa ajira,” amesema.
Katika awamu ya kwanza ya mradi huo, vijana 170 walihitimu na kukabidhiwa vyeti pamoja na vifaa vya kuanzia kazi.