SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha usimamizi wa mizigo inayoingia nchini kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi jirani ili kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar, alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika Idara ya Forodha kukagua namna ukusanyaji wa mapato unavyosimamiwa kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Balozi Omar amesema licha ya kuongezeka kwa mapato yatokanayo na forodha, bado kuna changamoto ya ukwepaji kodi kupitia mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya mipaka ya Tanzania. Amesema baadhi ya mawakala huingiza mizigo wakidai inapelekwa nchi jirani, lakini huishusha na kuisambaza ndani ya nchi kinyume cha taratibu. Kutokana na hali hiyo, aliitaka TRA kuimarisha ushirikiano na nchi zenye uhusiano wa kibiashara na Tanzania, ikiwemo China,

India na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Amesema hatua hiyo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho China imeondoa ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka barani Afrika. SOMA: Balozi Omar awataka TRA kuongeza makusanyo

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Fedha. Amesema katika kuimarisha udhibiti wa mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya mipaka ya Tanzania, TRA kupitia ving’amuzi na kamera zinazofungwa kwenye magari ya mizigo imefanikiwa kukamata matukio 16 ya ukiukwaji wa sheria yenye thamani ya Sh bilioni 3.2.

Ameongeza kuwa katika makosa 15 kati ya hayo, TRA imetoza faini ya Sh bilioni 2.5, huku shauri moja lililofikishwa mahakamani likiendelea kushughulikiwa. Katika ziara hiyo kwenye ofisi za TRA Dar es Salaam, Balozi Omar pia alitembelea Idara ya Forodha, Kitengo cha Ufuatiliaji wa Usafirishaji, Idara ya Upelelezi wa Kodi, Idara ya Kodi za Ndani na timu inayosimamia Mfumo Mpya Jumuishi wa Kodi za Ndani (IDRAS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *