
Kasi ya ongezeko la idadi ya wabunge wanawake duniani ni ya ‘mwendo wa kobe’ imesema ripoti mpya ikionesha ongezeko la mwaka jana 2025 la idadi yao kuwa ni 0.3 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Ripoti imesema “hadi tarehe 1 Januari 2026, wanawake walikuwa wanashikilia asilimia 27.5 ya viti katika mabunge ya kitaifa duniani kote, ikiwa ni ongezeko dogo kutoka asilimia 27.2 mwaka 2025. Ongezeko hili la asilimia 0.3 linaendana na kasi ya mwaka 2024, na hivyo kuashiria ukuaji wa polepole zaidi tangu mwaka 2017 kwa mwaka wa pili mfululizo.”
Katika maspika wapya 75 mwaka 2025 wanawake ni 12 pekee
Ingawa uwakilishi wa wanawake umeongezeka kidogo, idadi ya wanawake wanaoshika nafasi ya uspika wa mabunge imepungua kwa kiasi kikubwa. Uwiano wa wanawake maspika umeshuka hadi asilimia 19.9, sawa na maspika 54, ikilinganishwa na asilimia 23.7 mwaka mmoja uliopita.
Kati ya maspika 75 wapya walioteuliwa au kuchaguliwa mwaka 2025, wanawake walikuwa 12 pekee, sawa na asilimia 16.
Nchi zenye wanawake wengi kuliko wanaume kwenye bunge la juu au la chini
Kanda ya Amerika imeendelea kuongoza kwa uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake bungeni. Wanawake walikuwa asilimia 36.1 ya wabunge waliochaguliwa katika mabunge 20 ya nchi 13 zilizofanya uchaguzi wa wabunge mwaka 2025.
Kwa ujumla, wanawake walikuwa asilimia 35.6 ya wabunge wote katika kanda hiyo kufikia tarehe 1 Januari 2026.
Kanda ya Amerika pia ina nchi 4 kati ya 7 duniani ambazo zimefikia usawa wa kijinsia au kuwa na wanawake wengi zaidi kuliko wanaume katika bunge la chini au bunge la juu.
Nchi hizo ni Bolivia, Cuba, Nicaragua na Mexico. Nchi nyingine zilizofikia kiwango hicho ni Rwanda, Andorra na nchi za Falme za Kiarabu, (UAE).
Kwa upande wa maendeleo makubwa zaidi mwaka 2025, Kyrgyzstan iliongoza kwa kuongeza uwakilishi wa wanawake kwa asilimia 12.9 katika bunge lake. Ilifuatiwa na Saint Vincent na Grenadines kwa ongezeko la asilimia 12.3, na baraza la juu la Saint Lucia kwa ongezeko la asilimia 9.1.
Mchango wa mgao wa uwiano wa viti maalum
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mifumo ya mgao wa viti imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwakilishi wa wanawake bungeni.
Mfumo huo umeonekana kuwa na mafanikio hasa katika nchi kama Kyrgyzstan na Ecuador.
Mwaka 2025, mabunge yenye mfumo wa mgao wa viti ulioainishwa kisheria au wa hiari yalichagua au kuteua wastani wa asilimia 30.9 ya wanawake, ikilinganishwa na asilimia 23.3 katika mabunge yasiyo na mfumo huo.
Rekodi mpya katika baadhi ya nchi
Licha ya kasi ya polepole ya maendeleo kwa ujumla, nchi kadhaa zimeweka rekodi mpya za uwakilishi wa wanawake bungeni.
Nchini Australia, wanawake 69 walichaguliwa kati ya wabunge 150 mwaka 2025, na hivyo kuwapa wanawake asilimia 46 ya viti — kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa nchini humo.
Nchini Czech pia kulikuwa na matokeo ya kihistoria ambapo wanawake 67 walichaguliwa katika bunge la chini lenye wabunge 200, kutoka wanawake 50 mwaka 2021, na hivyo kuongeza uwiano wao kutoka asilimia 25 hadi karibu theluthi moja ya wabunge wote.
Uwiano wa wanawake katika Bunge la Taifa la Ecuador ulifikia asilimia 45 baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa.
Mwaka 2025 pia ulikuwa wa kihistoria kwa siasa za Japan, ambapo kwa mara ya kwanza nchi hiyo imepata Waziri Mkuu mwanamke. Baada ya uchaguzi wa mwezi Julai, uwakilishi wa wanawake katika baraza la juu ulifikia rekodi ya asilimia 29.4.
Nchi zinazobaki nyuma
Kwa upande mwingine, uwakilishi wa wanawake bado ni mdogo zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambapo wanawake wanashikilia wastani wa asilimia 16.2 ya viti vya mabunge.
Nchi tatu Oman, Tuvalu na Yemen hazina hata mbunge mwanamke katika bunge lao la chini au bunge la pekee.
Vurugu dhidi ya wanawake wanasiasa
Mwanzoni mwa mwaka 2025, IPU ilitoa utafiti kuhusu ubaguzi wa kijinsia, unyanyasaji na vurugu dhidi ya wanawake katika mabunge ya eneo la Asia na Pasifiki, ukiendeleza tafiti zilizowahi kufanywa katika maeneo ya Afrika na Ulaya.
Utafiti huo ulionesha kiwango cha juu cha vurugu, ambapo asilimia 76 ya wabunge wanawake waliripoti kukumbwa na vurugu za kisaikolojia.
Asilimia 76 ya wanawake waliohojiwa waliripoti kukumbwa na vurugu ikilinganishwa na asilimia 68 ya wanaume. Hali hii inayoongezeka inaweza kuwakatisha tamaa baadhi ya wanawake kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa na hivyo kuwa kikwazo kingine katika juhudi za kuongeza uwakilishi wa wanawake katika siasa.
Hata hivyo ripoti hiyo ilieleza kuwa baadhi ya nchi tayari zimeanza kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo. Kwa mfano, Tume ya Uchaguzi ya Ufilipino iliingilia kati baada ya wagombea wanaume kutoa matamshi ya kudhalilisha dhidi ya wagombea wenzao wanawake, huku Bunge la Colombia likipitisha sheria ya kuzuia na kuadhibu vurugu dhidi ya wanawake katika siasa.