YANGA imerejea nyumbani ikitokea mkoani Singida ilikokwenda kurudisha heshima ya ushindi, sasa kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves amefichua siri moja ambayo utaelewa kasi ya kufunga mabao kwa washambuliaji wake ilivyo.

Ndani ya kikosi cha Yanga kwa sasa inayeongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara ni Prince Dube mwenye sita akifuatiwa na Laurindo Aurelio ‘Depu’ aliyefunga matano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro amesema, siri ya washambuliaji hao kukimbizana kwenye kufunga kuna malengo kila mshambuliaji wake amempangia ndani ya kikosi hicho.

Licha ya kwamba amegoma kuweka wazi zaidi, Pedro amesema sio tu kwa Dube na Depu, bali kila mshambuliaji kikosini hapo atawajibika kutimiza malengo hayo ambayo yamegawanywa kulingana na muda ambao wanaupata kwenye mechi za timu hiyo.

“Hakuna kazi inayofanyika bila malengo, ni kweli tumeweka malengo kwa kila mshambuliaji, kuna idadi ya mabao ambayo anatakiwa kuhakikisha anaifikia au hata kuvuka,” amesema Pedro.

“Sio rahisi kuweka malengo sawa kwa washambuliaji wote, kwa kuwa kama unavyoona kuna wale ambao wanapata muda zaidi wa kucheza lazima hao malengo yawe makubwa, baada ya hapo kuna wale ambao hawapati sana muda nao kuna malengo tofauti, siwezi kukuambia malengo ya kila mmoja wao, hiyo ni siri ya ndani zaidi.

“Tunataka kuwa na uwajibikaji kwenye timu yetu, tuna wachezaji wazuri maeneo yote na mpaka sasa naona tunakwenda vizuri, kama tukiona kuna kitu hakipo sawa tunazungumza nao na wanashirikiana vizuri.

“Kitu bora zaidi ambacho nakiona ni namna wachezaji wanavyoshirikiana vizuri uwanjani, unaona kama huyu anadhani kuna mwenzake anaweza kufanya kitu bora zaidi kwenye kufunga anamsaidia.”

Aliongeza kuwa, washambuliaji hawana sababu ya kutofikia malengo  kutokana na kikosi kuwa na viungo bora huku timu ikicheza soka la kushambulia na kutengeneza nafasi  kibao.

“Ukiangalia timu yetu sasa unaona changamoto ni wachezaji wenyewe kufunga kwa kutumia nafasi ambazo tunatengeneza kwa kuwa wanazungukwa na viungo wazuri wenye ubunifu, kwenye mechi tulizocheza mpaka sasa ni mbili pekee ambazo hatukufunga bao lolote, moja kwenye Ligi ya Mabingwa na nyingine dhidi ya Simba juzi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *