Guterres
Katika ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema wanawake duniani bado wanakabiliwa na tofauti kubwa za kisheria.
“Duniani kote, wanawake wana takribani asilimia 64 tu ya haki za kisheria ambazo wanaume wanazo,” anasema Guterres, akibainisha kuwa sheria za kibaguzi zinaweza kuathiri karibu kila sehemu ya maisha ya mwanamke, ikiwemo umiliki wa mali, ajira, talaka na uhuru wa kusafiri. Na anatoa mfano kwamba katika zaidi ya nchi 40, ubakaji ndani ya ndoa bado hautambuliwi kama uhalifu.
Bwana Guterres pia ameonya kuhusu mwenendo unaotia wasiwasi ambapo mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi kubwa yanaanza kufutwa. “Katikati ya kuongezeka kwa utawala wa kiimla, kuyumba kwa kisiasa, na juhudi mpya za kuimarisha mfumo dume, mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi kubwa yanarudishwa nyuma kuanzia ulinzi bora wa wafanyakazi hadi haki za afya ya uzazi na ngono,” amesema. Amezihimiza nchi kutekeleza ahadi zao chini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, Makubaliano ya Beijing na ya Jukwaa la Hatua.
Azoulay
Akisisitiza hoja hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay amesema bado kuna tofauti kubwa za kijinsia katika elimu, ajira na upatikanaji wa rasilimali za kiuchumi.
“Tofauti hizi si tu kwamba si za haki, bali pia zinadhoofisha jamii zetu kwa ujumla,” amesema, akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, ubunifu na amani ya kudumu.
Kupitia programu zake, UNESCO inaendelea kusaidia nchi kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu, sayansi na utamaduni. Mipango hiyo ni pamoja na kusaidia mageuzi ya sera katika nchi 20, kusaidia watafiti wanawake kupitia programu ya L’Oréal-UNESCO “Kwa ajili ya wanawake”, pamoja na kutoa fursa za elimu kwa wasichana katika maeneo kama Afghanistan kupitia madarasa ya kusoma na kuandika, vipindi vya redio na mafunzo ya ujuzi wa kujipatia kipato.
Kiujumla viongozi hao wawili wamesisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “Haki. Haki ya Kisheria. Hatua. Kwa Wanawake na Wasichana Wote” inapaswa kuleta mabadiliko halisi. “Tusipokuwa sawa chini ya sheria, basi hatuko sawa,” anasema Bwana Guterres, akitoa wito wa kuondolewa kwa sheria na mila za kibaguzi ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata heshima, fursa na uhuru wanaostahili kila mahali duniani.