
Baraza la maulamaa nchini Iran, hapo jana walimchagua mtoto wa Ali Khamenei, Mojtaba kuwa kiongozi mpya wa juu wa kidini kumrithi baba yake aliyeuawa katika mashambulio ya mwanzo yaliyofanywa na Marekani na Israel.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Uteuzi wa Mojtaba, mmoja wa watu wenye misimamo mikali, unaonesha namna Tehran imechagua njia tofauti na Marekani.
Mojtaba Khamenei, alizaliwa Septemba 8, 1969, huko Mashhad, na ni mtoto wa pili wa Ali Khamenei, uteuzi wake unakuja ikiwa ni wiki moja imepita tangu Marekani na Israeli zianzishe vita dhidi ya taifa hilo la kiislamu.
Mojtaba mara nyingi anatajwa kama mtu msiri na wakati huo huo anatajwa kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika utawala wa nchi, ambapo pia najulikana kuwa na uhusiano wa karibu na Kikosi chenye nguvu cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambacho wengi wanaamini ndicho kinachofanya maamuzi ya nchi.
Kufuatia uteuzi wake, baraza la wataalamu limewataka raia wa Iran kusimama nyuma ya kiongozi wao mpya, licha ya kuwa anaonekana ni kiongozi atakayeendeleza urithi wa baba yake dhidi ya mataifa ya magharibi.
Mojtaba, ambaye amekuwa nyuma ya pazia katika uongozi wa taifa hilo na wala hajawahi kushika wadhifa wowote wa ofisi ya uma, anaelezwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya mabaraza yanayofanya maamuzi na hasa kikosi cha mapinduzi IRGC.
Ushawishi wake ulianza kuonekana zaidi katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2005, ambapo kiongozi huyu mpya anadaiwa kumsaidia Mahmoud Ahmadinejad kutoka kikosi cha IRGC kumshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Akbar Hashemi Rafsanjani.
Wakati uteuzi wake ukiwa umepokelewa kwa hisia mseto nchini Mwake, Marekani na Israel zimesisitiza kutomtambua kiongozi yeyote ambaye hatakuwa na baraza zao, Israel ikienda mbali zaidi na kusema kuwa atakuwa shabaha ya mashambulizi yanayoendelea, kauli ambayo imeungwa mkono na Rais Donald Trump aliyedai Mojtaba hatakuwa na maisha marefu.